Wabunge watapeliwa: Wamwaga fedha kusaka uwaziri, Ikulu yatoa kauli nzito kuwaonya, JK kutangaza Mawaziri wapya leo


IKULU imewaonya wabunge wenye uchu wa kuwa mawaziri na mawaziri wanaotaka kubaki kwenye madaraka hayo wasikubali kurubuniwa na matapeli wanaojifanya maofisa Usalama wa Taifa ambao wanawataka kutoa fedha ili wasaidiwe kupata uwaziri.

Onyo hilo limetolewa wakati Rais Jakaya Kikwete akitarajiwa kutangaza Baraza jipya la Mawaziri leo baada ya kuwang’oa mawaziri wanne na mmoja kufariki dunia.

Akizungumza na Tanzania Daima jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema hakuna sababu za wabunge kukubali kutapeliwa kwa ajili ya kusaka uwaziri kwani mwenye mamlaka ya uteuzi ni Rais Kikwete na hakuna mwenye uwezo wa kuingilia uteuzi wake au kumshawishi afanye upendeleo.

Mbali ya kuwaonya wabunge na mawaziri hao, Balozi Sefue pia aliwaonya matapeli wanaotumia jina la Ofisi  ya Rais Ikulu kujifanya maofisa wa Idara ya Usalama kuwarubuni watoe fedha ili wawasaidie kuingia kwenye Baraza jipya la Mawaziri.

Kwa mujibu wa Balozi Sefue, wabunge wanapaswa kuwapuuza matapeli hao na kufahamu kuwa Ikulu haitahusika na upotevu wowote wa fedha watakazotoa.

“Hao ni matapeli kama walivyo matapeli wengine, hakuna mtumishi wa Ikulu anayeweza kufanya jambo hilo na ninaomba watakaokutana na vitendo hivyo watoe taarifa polisi,” alisema Balozi Sefue.

Wakati Ikulu ikitoa taarifa hiyo, tayari baadhi ya wabunge na mawaziri wenye hofu ya kutorejea madarakani, wameingizwa mkenge kwa kutoa kati ya sh milioni 5 hadi 10 kwa watu waliojitambulisha kwao kama maofisa usalama walio karibu sana na rais, wanaochambua sifa za watu wanaofaa kuwa mawaziri na kuwasilisha majina na sifa zao kwa Rais Kikwete.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa matapeli hao wamekuwa wakiwapigia simu baadhi ya wabunge ambao wamekuwa wakitajwa mara kwa mara kwenye vyombo vya habari kuingia kwenye baraza jipya na kuwataka watoe kati ya sh milioni 5 hadi 10.

Mmoja wa wabunge ambaye hakupenda jina lake litajwe, alisema kuwa matapeli wamekuwa na mbinu nyingi na wamefanikiwa kuwaumiza baadhi ya wabunge kwa kuwalaghai watoe fedha.
“Utapeli wa aina hii umekuwepo nchini kwa kipindi kirefu na watu hao wana mbinu nyingi za ulaghai, hasa kwa wabunge  wenye uchu na nafasi hizo. Lakini si wabunge wote watakaoingia kwenye mtego huo maana wengi wameshashituka,”  alisema mbunge huyo.
Alisema kuwa utapeli wa aina hiyo umetumiwa hata katika vyombo vya dola pale wanapobaini kuwa kuna nafasi za kupandishwa vyeo kwa maofisi wa vyombo hivyo, matapeli hao hutumia fursa hiyo kujipatia fedha.
Mbali ya matapeli kutumia mwanya huo kuchota pesa, hivi sasa kumekuwa na sarakasi nyingi miongoni mwa wabunge, huku wengine wakichafuana ili kutwaa madaraka hayo makubwa kisiasa.

Habari zaidi zinasema kuwa Rais Kikwete leo anatarajiwa kutangaza Baraza jipya na hivyo kumaliza minong’ono ya muda mrefu juu ya muundo wa Baraza hilo.

Habari zinasema mawaziri hao endapo watatangazwa leo, wanapishwa kesho kutwa katika Ikulu ya Rais Kikwete. Katika mabadiliko hayo ambayo yanasubiriwa kwa shauku kubwa, Rais Kikwete anatarajia kujaza zaidi ya nafasi kumi mpya, nne zikitokana na mawaziri waliong’olewa hivi karibuni kutokana na tuhuma na kashfa zilizoibuka wakati wa Operesheni Tokomeza Ujangili.

Mawaziri waliokumbwa na kimbunga hicho na wizara zao kwenye mabano ni Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), David Mathayo (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi) na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi.

Rais Kikwete pia atakuna kichwa kumpata Waziri wa Fedha na Uchumi atakayeziba nafasi ya marehemu William Mgimwa, aliyefariki dunia Januari mosi nchini Afrika Kusini alikokuwa akipata matibabu.
Rais Kikwete pia atalazimika kuwatema baadhi ya mawaziri waliopendekezwa na Kamati Kuu(CC) ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) kwamba wang’olewe kwa madai kuwa ni mizigo.

Kundi la mawaziri mizigo wamo Waziri wa Kilimo na Chakula, Christopher Chiza, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa,Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia.

Katika mabadiliko hayo, rais anatarajia pia kuwatema au kuwahamisha wizara mawaziri walio nje ya kundi la ‘mizigo’  ambao wameshindwa kuendana na kaulimbiu ya ‘Kasi mpya, ari mpya na nguvu mpya.’
Katika kundi hili, Rais asipowang’oa anaweza kuwabadilisha wizara kutoka moja kwenda nyingine.
Katika kundi hili, yumo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ambaye amekuwa akilalamikiwa kwa utendaji usiokidhi viwango tangu aingie madarakani.

Wengine ni Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka. Duru za siasa zinamwelezea Waziri Tibaijuka kama waziri aliyeshindwa kuimudu wizara hiyo, tofauti na matarajio ya wengi kutokana na kuibuka kwa migogoro mingi iliyosababisha mauaji ya watu wengi nchini.

Maeneo yaliyokumbwa na migogoro mikubwa ya ardhi na ambayo hadi sasa imeshasababisha mauaji ya kinyama ni pamoja na mgogoro katika eneo la Kiteto, Kapunga, Mvomero, Mtibwa, Malinyi, Kilombero na kwingineko.

Chanzo: Tanzania Daima

Comments

Popular

GIDABUDAY KUHAMASISHA UJENZI WA KIJIJI CHA MICHEZO TANZANIA LENYE JINA YA MWANARIADHA MKONGWE BW.JOHN STEPHEN AKHWARI

Rio Olympics: Brazil win men's volleyball gold, GB's Joyce takes boxing silver – as it happened

Olympics 2016: Usain Bolt completes sprint double, Jade Jones retains taekwondo title

Rio Olympics: Swimmer Lochte apologises for 'robbery' saga