Latest News

Monday, February 17, 2014

Kili Marathon yatangaza njia mpyaWAANDAAJI wa Kilimanjaro Marathon wametangaza njia mpya zitakazotumika mwaka huu, ikiwa ni hatua nyingine muhimu katika mafanikio ya mbio hizo ambazo zinaingia mwaka wa 12 tangu kuanzishwa.

Njia hizo mpya zimelenga kuboresha mwendo wa washiriki barabarani na kuwafanya wafurahie zaidi mbio hizo zilizopangwa kufanyika Machi 2 mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Akitangaza njia hizo mpya jana, John Addison, Mkurugenzi wa Wild Frontiers, waandaaji wa mbio hizo, alisema wameanzisha njia mpya ili kuzuia msongamano wa watu wakati wa mbio kutokana na kuongezeka idadi ya washiriki kila mwaka.

Addson alisema washiriki wa mbio ndefu za marathon km 42, nusu marathon km 21, mbio za walemavu na mbio za kujifurahisha za Vodacom 5km Fun Run, sasa hawatapishana tena barabarani, bali kila njia itatiririka katika muelekeo mmoja.

“Pia kutokana na mabadiliko haya, washiriki watakuwa wameepuka kilomita 3 za mwinuko mkali kuelekea Chuo cha Mweka ambapo awali ndipo palikuwa mahali pa kugeuzia washiriki wa mbio za full marathon na half marathon.

“Mbio za walemavu za Gapco ambazo zitakuwa na makundi mawili tu mwaka huu ya kiti cha magurudumu (wheelchair), na baiskeli ya mikono (handcycle), zimefupishwa kutoka half marathon na kuwa km 10 ili kutoa fursa kwa watu wengi zaidi kushiriki, na njia sasa itapita eneo tambarare na lenye kivuli,” alisema.

Alisema mbio ndefu za Kilimanjaro Premium Lager 42 km marathon zitaanza saa 12.30 asubuhi kutokea uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika na Biashara (MUCCoBS), na kupita barabara iendayo Dar es Salaam kwa kilomita kumi na kurudia geti la Ushirika halafu zitakwenda kilomita 8 kuelekea Hospitali ya KCMC na kukata kushoto hadi Barabara ya Lema (Lema Road).
 
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa nusu marathon zitaanza saa moja kamili asubuhi kutokea MUCCoBS na kupandisha kaskazini kuelekea Hospitali ya KCMC kwa kilomita 8 ambazo ni sawa na ongezeko la mwinuko wa futi 250 kutoka usawa wa bahari, kisha zitapita Lema Road na kurudi uwanjani.

Mbio za walemavu za Gapco Disabled 10 km marathon zitaanzia uwanja wa MUCCoBS na kufuata barabara ya Kilimanjaro hadi Lema Road na kugeuza.

Addison alisema Vodacom 5km Fun Run zitaanzia mzunguko wa YMCA upande wa Barabara ya Arusha na zitakwenda hadi kwenye mnara wa saa na kupita Boma Road kuelekea mzunguko wa Barabara ya Arusha na mzunguko wa YMCA tena na watapita Uru Road na kuingia uwanjani kupitia geti la mashariki.

Executive Solutions ni waratibu wa mbio za Kilimanjaro Marathon 2014 wakishirikiana na Riadha Tanzania (RT), Chama cha Riadha Kilimanjaro na Kilimanjaro Marathon Club huku zikidhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager (wadhamini wakuu), Vodacom Tanzania, GAPCO, Simba Cement, KK Security, Keys Hotel, TPC Sugar, TanzaniteOne, CMC Automobiles Ltd, RwandAir, FNB Tanzania, UNFPA na Kilimanjaro Water.

CHANZO: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment