Wanariadha mashuhuri kuchuana Kili Marathon


John Bayo/Mwingereza/Musa Ninga
WANARIADHA mashuhuri wa Tanzania wanatarajiwa kupambana vilivyo ili kutwaa medali na fedha katika mbio za Kilimanjaro Marathon 2014 zinazotarajiwa kufanyika Machi 2 mjini Moshi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa mbio hizo, John Bayo, wanariadha maarufu wa Tanzania, Andrew Sambu, John Leonard na Daudi Joseph ni miongoni mwa wanariadha Watanzania watakaoshiriki katika mbio za Km 42 kwa wanaume.

Katika mbio za kilomita 42 kwa wanawake, watakuwepo Banuelia Brighton, Fabiola William na Flora Yuda, ambao wanatarajiwa kutoa upinzani mkali kwa wanariadha wengine Watanzania pamoja na wa kigeni.
Andrew Sambu ana rekodi ya kumaliza Korea Marathon kwa saa 2:09:52 mwaka 2004 na mshindi wa medali ya fedha kwenye Mashindano ya Riadha barani Afrika na ameshiriki Olimpiki, wakati Banuelia Brighton akiwa ameshinda Kigali Peace Marathon mwaka 2009 na kumaliza wa pili Kampala Marathon mwaka 2011.

Dickson Marwa, mshindi wa Ngorongoro Half Marathon 2013 ambako alimaliza wa kwanza akitumia saa 1:4:49, Alphonce Felix pamoja na Ezekiel Jafari ni kati ya wanariadha ambao wataiwakilisha Tanzania kwenye mbio za Km 21 kwa wanaume huku kwa wanawake wakitarajiwa Mary Naali, Jacqueline Sakilu na Sarah Ramadhani.

Akiwa ametengeneza rekodi nyingi, Mary Naali ni kati ya wanariadha bora nchini katika mbio za Km 21 maarufu kama Half Marathon. Alishinda Vienna Marathon mwaka 2010 akitumia saa 1:12:16 na baada ya hapo akavunja rekodi kwenye mbio za kilomita 25 za Arusha VIP Race mwaka 2011 akitumia saa 1:20:52 na kuvunja ile ya 1:22:18 iliyokuwa imewekwa na Josephine Deemay mwaka 2006. Mei mwaka 2013 pia alishinda mbio ya Bucharest International Marathon huko Romania akitumia saa 1:16:32.

Naali atashindana na Sarah Ramadhani ambaye ni bingwa mtetezi kutokana na ushindi wake kwenye Kilimanjaro Marathon 2013 alipomaliza akitumia saa 1:13:05. Pia katika mchuano huo, atakuwemo Jacqueline Sakilu, ambaye ni kati ya wanariadha wanaotarajiwa kufanya makubwa baada ya kushinda mbio kadhaa za kilomita 21, ikiwemo Uhuru Marathon 1:15:25 na Ngorongoro Run 1:16:50.

“Tuna furaha kuwa na kikosi madhubuti kwa wanaume na wanawake. Uwepo wa wanariadha hawa wazoefu, naamini utaifanya mbio hii iwe ya kuvutia,” alisema John Bayo ambaye pia ni kocha maarufu wa riadha.
“Wanariadha wetu wana viwango vya kimataifa. Baadhi ya wanariadha wa kiume wameishakimbia chini ya muda wa saa 2:15:00 huku upande wa wanawake wakiwa wamekimbia chini ya 2:40:00. Hii ni mbio ya kimataifa, ambapo mshindi anaweza kuwa mtu yeyote kutoka taifa lolote, lakini kinachotupa nguvu ni hamasa tunayoipata kutoka kwa wananchi, maana mbio inafanyika hapa nyumbani, hivyo basi tuko tayari kwa changamoto hii,” alisema.
Naye Aggrey Marealle, Mkurugenzi Mkuu wa Executive Solutions, waratibu wa mbio hizo, alithibitisha kwamba, timu ya wanariadha inayoandaliwa na Holili Athletics Club, imekuwa katika maandalizi kwa miezi minane iliyopita na wako tayari kupeperusha bendera ya Tanzania. Timu hiyo imepunguzwa kutoka wanariadha 20 hadi wanane bora, ambao wako kwenye maandalizi ya mwisho.

Kwa upande wake, John Addison, Mkurugenzi Mkuu wa Wild Frontiers ambao ndio waandaaji wa mbio hizo, alisema, takriban washiriki 6,000 kutoka nchi zaidi ya 40 duniani wanatarajiwa kushiriki kwenye mbio za 12 za Kilimanjaro Marathon.

Kilimanjaro Marathon 2014 inaratibiwa na Executive Solutions kwa ushirikiano na Riadha Tanzania (RT), Chama cha Riadha Mkoa wa Kilimanjaro na Kilimanjaro Marathon Club zikidhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager (wadhamini wakuu), Vodacom Tanzania, GAPCO, Simba Cement, KK Security, Keys Hotel, TPC Sugar, TanzaniteOne, CMC Automobiles Ltd, RwandAir, FNB Tanzania, UNFPA na Kilimanjaro Water.

CHANZO: Tanzania Daima


Comments

Popular

GIDABUDAY KUHAMASISHA UJENZI WA KIJIJI CHA MICHEZO TANZANIA LENYE JINA YA MWANARIADHA MKONGWE BW.JOHN STEPHEN AKHWARI

Rio Olympics: Brazil win men's volleyball gold, GB's Joyce takes boxing silver – as it happened

Olympics 2016: Usain Bolt completes sprint double, Jade Jones retains taekwondo title

Rio Olympics: Swimmer Lochte apologises for 'robbery' saga