Latest News

Tuesday, March 4, 2014

Jackline Sakilu, nyota anayechipukia riadha JWTZ

JESHI la Wananchi Tanzania (JWTZ), ni miongoni mwa taasisi ambazo kutokana na asili ya utendaji wake, imekuwa ikishiriki katika michezo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Kuna madhumuni yanatoa kipaumbele cha michezo jeshini. Baadhi yake ni kujenga na kukomaza afya ya mwili, akili na maisha bora kwa mafisa na askari. Kujenga ukakamavu, nidhamu na uwezo  binafsi wa kujihami katika jamii na taifa kwa ujumla. Hali kadhalika kujenga tabia ya ushirikiano, upendo, umoja na uzalendo miongoni mwa wanajeshi wenyewe na jamii nzima. 
Aidha, imechangia sana katika kutambua, kubaini na kuendeleza vipaji kwa wanajeshi na wananchi kwa ujumla, kuwapatia burudani na kuitangaza Tanzania kimataifa, pamoja na  kujenga uhusiano mzuri wa majeshi ya nchi rafiki,   na mengine duniani.
Lakini pia kutekeleza maazimio ya shirikisho la michezo ya majeshi duniani (CISM) ambayo ni  kutumia michezo kama zana ya kueneza amani duniani badala ya vita, hivyo kuitekeleza kauli mbinu ya urafiki kupitia michezo na mwisho kulifanya jeshi kuwa kitalu cha maendeleo ya michezo nchini.
Mchezo wa riadha ni miongoni mwa michezo kadhaa inayopewa kipaumbele ndani ya JWTZ.
JWTZ, liliwahi kutoa wanariadha nyota wa kitanzania kama Philbert Bayi, Juma Ikangaa na wengine wengi katika miaka ya 1970.
Baada ya nyota hawa kustaafu mchezo huo, imepita miaka kadhaa Tanzania haikupata nyota wa riadha kama hao. Kuna  baadhi ya wadau wa mchezo huo waliofikia hatua ya kusema kuwa pengine mchezo huo unaelekea kupotea kabisa katika ramani ya taifa hili.
Hivi karibuni, JWTZ limevumbua kipaji kingine kipya katika mchezo wa riadha.
Private Jackline Sakilu, mzaliwa wa mkoa wa Singida alianza mchezo huu akiwa na umri mdogo kabisa wa miaka tisa hivi ikiwa ni ngazi ya shule ya msingi, kata, kanda na hatimaye ngazi ya kitaifa (UMITASHUMTA). Jackline anasema kuwa, mara baada ya kumaliza elimu yake ya msingi  alichaguliwa kujiunga na klabu ya riadha iliyopo mkoani Arusha kwa ajili ya kufanya mazoezi ya mchezo huo, nia ikiwa ni kuendeleza kipaji chake.
Akiwa katika kambi hiyo, kwa mara ya kwanza alifanikiwa kuiwakilisha nchi katika mashindano ya mbio za nyika za Dunia yaliyofanyika Ufaransa na kushika nafasi ya 32 kidunia.
Hivi karibuni katika kusherehekea miaka 52 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Alishika nafasi ya kwanza katika Mashindano ya Uhuru Marathon katika mbio za kilomita 21.
Pia alikuwa mshindi wa kwanza katika Marathon iliyoandaliwa na Dar Rotary Marathon kwa upande wa wakimbiaji wa kike iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Octoba 2013.   Baada ya hapo alishiriki katika mashindano ya Afrika Mashariki nchini Uganda katika mbio za Mita 800 na kushika nafasi ya nne.
Mwaka 2005 alishika nafasi ya kwanza kwenye mashindano ya Taifa ya Riadha Dodoma, katika mbio za Mita 800 na 1500.  Huo ukawa mwanzo wa mafanikio makubwa kwa Jackline.
Mwaka 2009 JWTZ lilitangaza ajira kwa watanzania wenye vipaji vya mchezo wa riadha kujiunga na jeshi ili kuendeleza vipaji vyao.
Taarifa hizo bila shaka zilikuwa njema kwa Jackline, ambaye kwa  wakati huo alikuwa na hamu ya kuendeleza kipaji chake. Mwaka 2010 alihitimu mafunzo ya awali na kufanikiwa kujiunga na JWTZ na baadaye akajiunga na timu teule ya jeshi ya mchezo huo.
Baadaye mwaka 2012, Jackline aliliwakilisha JWTZ kwenye michezo ya Majeshi ya Dunia, (CISM) iliyofanyika Rio de Janeiro, Brazil na kufanikiwa kushika nafasi ya nne katika mbio za kilomita 800. Mwaka 2012, aliliwakilisha tena JWTZ katika michezo ya Majeshi kwa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki huko Burundi. Alishika nafasi ya tatu katika mbio za Nyika za Kilomita nane kwa upande wa wanawake.
Hivi karibuni, Jackline alishiriki katika mashindano ya kimataifa ya riadha nchini Brazil, yakihusisha nchi za Kenya, Ethiopia, Ujerumani, Italia, Tanzania na Brazil.
Katika mashindano hayo ambayo yalishirikisha jumla ya washiriki 900, Jackline aliibuka na medali saba za dhahabu na moja ya fedha.
Katika mashindano hayo, Jackline amelipatia heshima kubwa JWTZ na taifa kwa ujumla, na kuacha gumzo nchini Brazil baada ya kuvunja rekodi zake kadhaa katika mashindano hayo kwa kukimbia mwendo wa kasi zaidi kuliko ule wa awali.
Katika mbio za kilomita 21 na kilomita 10, alitumia dakika 71 na sekunde 28,  tofauti na awali ambapo alitumia dakika 73 na sekunde 17. Mbio za kilomita 10 alitumia dakika 33 na sekunde 15, wakati awali alitumia dakika 34 na sekunde 4.
Jackline anasema pamoja na kuzingatia mazoezi, mafanikio hayo ni kutokana na malezi bora ya kukuza vipaji ndani ya JWTZ pamoja na kuzingatia maelekezo anayopata kutoka kwa kocha wake aliyemtaja kuwa ni Sajini Shaban Hiki.
Aidha, mbali na mchezo wa riadha, Raia Mwema lilitaka kujua ushiriki wa JWTZ katika michezo mingine, jitihada zinazochukuliwa na jeshi hilo katika kukuza michezo mingine. Msemaji wa Jeshi, Luteni Kanali Erick Komba amefafanua; “JWTZ limekuwa likishiriki katika Michezo ya Kimashindano na michezo kwa wote.
“Michezo ya Kimashindano huhusisha ushiriki wa wanajeshi katika michezo ya kimashindano kitaifa  na kimataifa. Ushiriki huu hufanywa na timu teule ya JWTZ katika mashindano mbalimbali yanayosimamiwa na mashirikisho husika ya michezo nchini kama vile TFF kwa Mpira wa Miguu na vyama vingine,”
Aidha, anaendelea kusema kuwa, JWTZ pia hushiriki katika michezo inayoandaliwa na Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA). JWTZ pia linasimamia Kituo cha Kukuza na Kuendeleza Vipaji katika Michezo cha Twalipo Camp Youth Sports Foundation.
Pamoja na JWTZ kushiriki kikamilifu michezo ndani ya nchi, limeshiriki pia katika michezo mbalimbali kimataifa, kama vile mashindano yanayoandaliwa na mashirikisho ya Michezo ya Majeshi ya Dunia (CISM) ambapo mwaka huu Tanzania itakuwa mwenyeji wa mashindano hayo ambayo huhusisha karibu michezo yote kulingana na hali ya uchumi kwa nchi mwenyeji.
Anasema kuwa, kwa ujumla michezo hii hulenga kustawisha na kudumisha utimamu wa mwili na viungo kwa wanajeshi wote.
Ushiriki wa JWTZ katika michezo ya kimashindano ulianza mara baada ya vita ya Kagera 1979/80, ambapo ziliundwa timu za jeshi.
Hii ilifanyika kwa michezo baina ya vikosi na vikosi na hivyo  kuteua wachezaji wenye viwango vya kitaifa na kimataifa na kuunda timu teule za Jeshi. Timu za kwanza zilikuwa ni za mpira wa Kikapu na Pete.
Chanzo: Raia Mwema


No comments:

Post a Comment