KIKATIBA YEYE NANI? Kibali ujenzi Yanga mwisho wa mwezi

Mzee Ibrahim Akilimali
WAKATI Wazee wa Klabu ya Yanga wakipiga mkwara wa kutaka ndani ya siku tano wawe wamepewa kibali cha ujenzi makao makuu ya klabu yao Jangwani, Halmashauri ya Ilala imesema jambo hilo litaanza kufanyiwa kazi mwishoni mwa mwezi huu.
Juzi, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi ya Yanga, Francis Kifukwe, alilalamika kuwa, licha ya kutuma maombi muda mrefu Manispaa ya Ilala kuomba kibali cha ujenzi pamoja na kuongezewa eneo, lakini wahusika wamekuwa kimya na kibaya zaidi, waliwafukuza kwenye kikao cha juzi.
Wakati Kifukwe akilalamika juzi, jana Katibu wa Baraza la Wazee wa Yanga, Ibrahim Akilimali, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kwamba, wanampa siku tano Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, kuhakikisha wanatoa kibali kwa klabu hiyo kuanza ujenzi wa uwanja unaotarajiwa kuitwa ‘Jangwani City’.
Akizungumza kwa mbwembwe, Akilimali alisema, wanatoa siku hizo kuhakikisha Silaa anatoa kibali, bila hivyo watahakikisha wanamwaga mboga, kwani ugali wameumwaga wao.
“Tunajua manispaa inatuwekea kauzibe, na sisi Yanga ni klabu kubwa na inafahamika toka enzi za Karume, hivyo basi, manispaa inamwaga mboga na sisi tutamwaga ugali endapo siku tano tulizozitoa zitakosa majibu,” alisema Akilimali aliyejitapa kupewa ruhusa ya kuzungumza na waandishi wa habari baada ya hivi karibuni kupigwa ‘stop’ na mwenyekiti wa klabu hiyo.
Aidha, Akilimali alisema, mbali na kumwaga mboga, wameazimia kufanya maandamano, ambayo yatamlenga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mecky Sadick, Silaa na Rais Jakaya Kikwete.
Wakati hali ikiwa hivyo, Manispaa ya Ilala imekiri kupokea maombi ya kuomba kibali kutoka uongozi wa klabu ya Yanga juu ya kutaka kuuboresha uwanja wa timu hiyo uliopo eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Halmashauri hiyo, Lucy Semindu, alisema kuwa kamati ya mipango miji na mazingira ya halmashauri hiyo ilipokea maombi hayo.
Semindu alisema kuwa, kamati hiyo itaanza ukaguzi wa eneo hilo mwishoni mwa mwezi huu ili kuhakikisha wanajiridhisha kabla ya kuanza kwa ujenzi huo.
“Uongozi wa timu hiyo uliwasilisha maombi ya kuomba kibali cha ujenzi kwa ajili ya uwanja huo, ambayo yamepokewa rasmi na kamati husika, ambayo wiki ijayo itafanya ziara kukagua eneo hilo,” alisema.
Alisema kuwa baada ya kuridhika na ukaguzi huo, halmashauri hiyo itatoa kibali hicho mwishoni mwa mwezi huu.
CHANZO: Tanzania Daima



Comments

Popular

GIDABUDAY KUHAMASISHA UJENZI WA KIJIJI CHA MICHEZO TANZANIA LENYE JINA YA MWANARIADHA MKONGWE BW.JOHN STEPHEN AKHWARI

Rio Olympics: Brazil win men's volleyball gold, GB's Joyce takes boxing silver – as it happened

Olympics 2016: Usain Bolt completes sprint double, Jade Jones retains taekwondo title

Rio Olympics: Swimmer Lochte apologises for 'robbery' saga