Latest News

Tuesday, March 4, 2014

SOKA LA VIJANA: Kocha Manyara aipania Arusha

KOCHA wa Kombaini ya Mkoa wa Manyara, Mohamed Ismail, ametamba kujibua mapigo dhidi ya Arusha katika mchezo wa maruadiano wa kusaka vipaji vya nyota wa kuboresha timu ya taifa ‘Taifa Stars’ ambayo imeonekana kutofanya vema katika mechi zake mbalimbali.
Mchakato huo wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Rais wake, Jamal Malinzi, wenye lengo la kuibua vipaji, ulianza Februari 22 katika mikoa yote hapa nchini.
Kauli ya Ismail, imekuja baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa wenyeji wao Arusha ambao walionyesha kandanda safi na la kuvutia katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abed jijini hapa juzi.
Ismail alisema ana imani kubwa ya kushinda katika mchezo wa marudiano utakaopigwa kesho kwenye uwanja wa Babati mkoani Manyara na kudai kuwa, bao moja la ugenini ni faraja kubwa kwake.
“Leo tumefungwa si kusema vijana wangu si wazuri, bali wapinzani wetu wameyatumia makosa yetu na kushinda mchezo huu, ila kusema kweli mashindano haya ya kusaka vipaji kama Malinzi angeingia miaka kadhaa madarakani, nina imani tungekuwa mbali kisoka,” alisema Ismail na kuongeza kuwa, nyota wa kuunda kikosi chake aliwakusanya kutoka katika academy mbalimbali mkoani kwao kama vile Mei, VITC, Veta, Usalama pamoja na Babati Rangers.
Naye Kocha wa Arusha, David Nyambele, aliwapongeza vijana wake kwa kujituma hadi kuibuka na ushindi huo, huku akijivunia kuwa na nyota wengi wazuri katika kikosi chake.
“Mimi kikosi changu kina wachezaji wazuri na wana uwezo wa hali ya juu, pia hakuna anayezidi miaka 25, hivyo basi mimi binafsi naviona vipaji vingi hapa nchini na si kuangalia wachezaji wa timu kubwa pekee,” alisema.
Michuano hiyo ya kusaka nyota wa kuboresha Taifa Stars inatarajiwa kufikia tamati kesho.
CHANZO: Tanzania Daima


No comments:

Post a Comment