Fabian Joseph, Jackline Sekilu mabingwa Sokoine Min Marathon 2014



BINGWA wa mbio za Edmund World Half Marathon nchini Canada mwaka 2005, Fabian Joseph, na bingwa wa Kili Marathon 2014 kwa wanawake, Jackline Sekilu, wameibuka washindi wa Sokoine Min Marathon 2014, katika mashindano ya Kumbukumbu ya Miaka 30 ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, hayati Edward Moringe Sokoine, yaliyofanyika jana mjini hapa.

Fabian aliibuka mshindi wa kwanza wa mbio hizo za kilometa 10 kwa kutumia dakika 34:28:04 na kufuatiwa kwa karibu na Alphonce Frank wa Shule ya Winning Spirit aliyetumia dakika 34:41:89 na nafasi ya tatu ikiangukia kwa mwanariadha Dickson Marwa wa Holili, aliyetumia dakika 34:57:47.

Kwa kuibuka kidedea, Fabiani amezawadiwa fedha taslimu shilingi 500,000, kombe, medali na cheti maalum, wakati mshindi wa pili akipata shilingi 400,000, medali na cheti, huku mshindi wa tatu akipata shilingi 300,000, medali na cheti.

Wanariadha wengine waliomaliza katika kumi bora na timu zao kwenye mabano ni Gabriel Gerald (Wining Spirit), Fabiani Nelson (CCP Moshi), Pascal Sarwat (Holili), Andrea Samba (Wining Spirit), Nyangero Patrick (Arusha), Shanga Gitina (ACSC) na John Leonard (Wining Spirit).

Kwa upande wa wanawake, Jackline Sekilu alitumia dakika 40:01:26, wakati nafasi ya pili ikienda kwa Natalia Elisante (40:51:27), Failuna Abdi (41:13:59) na kufuatiwa na bingwa wa zamani wa Kili Marathon, Mary Naali aliyeshika nafasi ya nne na wa tano akimaliza Selina Amos kutoka Zanzibar.

Kwa upande wa mbio za walemavu, washindi wa kwanza hadi wa tatu walitoka Dar es Salaam ambao pia walikimbia kilometa 10, ambapo nafasi ya kwanza ilikwenda kwa Wilbert Costantino, wa pili Shukuru Halfani na wa tatu alikuwa ni Mathias Solo.

Mashindano mengine yaliyopamba maadhimisho hayo ya Sokoine Day 2014 ni pamoja na kutupa mkuki na kuruka juu (Long Jump) na washindi wa kurusha mkuki walikuwa ni Said Thomas aliyefuatiwa na Samson Kaura na Julius Daniel alikuwa wa tatu.

Kwa upande wa kuruka juu, Michael Gwandu alikuwa wa kwanza kwa kuruka meta 6.80, akifuatiwa na Michael Danford aliyeruka mita 6.37 na Kalum Said alikuwa wa tatu kwa kuruka mita 5.27.

Mmoja wa wadhamini wa mbio hizo, Lulu Lengele alisema kuwa mfuko wa PPF wameamua kudhamini sehemu ya mbio hizo kwa kutoa zawadi zote walizopewa washindi na wataendelea kudhamini mbio hizo na michezo mingine kama sehemu ya afya kwa wananchi.

Wadhamini wengine wa mbio hizo walikuwa ni Kampuni ya Mega Trade kupitia kinywaji cha K-Vant Gin iliyowakilishwa na Meneja Masoko wake Goodluck Kway, ambaye aliridhisha na mashindano hayo na kuahidi kuendelea kuyafadhili kwa miaka ijayo.

Alipokuwa akikabidhi zawadi hizo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, alisema kuwa huo ndio uzalendo unaotakiwa katika kuwaenzi mashujaa kama Sokoine, hivyo kuwataka Watanzania kutomlilia huku wakiacha kufuata mema aliyokuwa akitenda, pamoja na kuendeleza aliyoyaacha.

CHANZO: Tanzania Daima


Comments

Popular

GIDABUDAY KUHAMASISHA UJENZI WA KIJIJI CHA MICHEZO TANZANIA LENYE JINA YA MWANARIADHA MKONGWE BW.JOHN STEPHEN AKHWARI

Rio Olympics: Brazil win men's volleyball gold, GB's Joyce takes boxing silver – as it happened

Olympics 2016: Usain Bolt completes sprint double, Jade Jones retains taekwondo title

Rio Olympics: Swimmer Lochte apologises for 'robbery' saga