Latest News

Thursday, May 15, 2014

Taswa kuandaa mjadala Jumuiya ya Madola

CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (Taswa), kimeanzisha utaratibu wa kuandaa midahalo mbalimbali ya masuala ya michezo kila Jumatano ya kwanza ya mwezi, ambapo kwa kuanzia wataanza na uwakilishi wa Tanzania katika michezo ya Jumuiya ya Madola.
 
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Taswa, Amir Mhando, watakuwa wakialika wataalamu kutoka vyama vya michezo, wanamichezo maarufu, wahariri wa habari za michezo na waandishi wa habari za michezo, ambao watakuwa wakijadili hoja husika.

Alisema huo ni uamuzi wa Kamati ya Utendaji iliyokutana Jumatatu, ambapo mambo mbalimbali yalijadiliwa, na kuongeza kuwa kutakuwa na wazungumzaji maalumu kuhusu mada husika, ambapo wageni waalikwa watachangia kwa nia ya kuboresha kwa maslahi ya ustawi wa michezo hapa nchini.

Mhando alisema kwa kuanzia mjadala huo utafanyika Juni 4 katika ukumbi ambao utatangazwa hivi karibuni, na mada itakuwa nafasi ya Tanzania katika Michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Glasgow, Scotland kuanzia Julai 23 hadi Agosti 3.

Tanzania itashiriki katika michezo ya ngumi, riadha, kunyanyua vitu vizito, mpira wa meza, judo na kuogelea, ambapo wachezaji tayari wapo katika maandalizi kwa lengo la kufanya vizuri kwa heshima ya nchi.

Alisema mbali ya viongozi wa vyama mbalimbali vya michezo, pia utaratibu unalenga kuwaalika baadhi ya Watanzania waliopata medali katika mashindano hayo, ili nao waweze kuzungumza na kuwahamasisha wanamichezo wa sasa wafanye vizuri.

Kuhusu tuzo za wanamichezo bora, Mhando alisema Kamati ya Utendaji imepongeza juhudi zinazofanywa na Kamati ya Tuzo za Wanamichezo Bora inayoongozwa na Mkurugenzi wa Radio Times FM, Rehure Nyaulawa, katika kuhakikisha zinakuwa bora na za aina yake mwaka huu.

Alisema tayari wadau kadhaa wameonyesha nia ya kudhamini tuzo hizo, ambapo maelezo zaidi yatatolewa baada ya kikao cha Kamati ya Tuzo kufanyika Jumatatu wiki ijayo kujadili maendeleo kuhusiana na tuzo hizo.


Juu ya Saccos, alisema kikao kimeteua wanachama sita wa Taswa, kuratibu na kuandaa Katiba ya Chama cha Akiba na Mikopo (Saccos), kwa ajili ya wanachama na kusimamia uanzishwaji wake.

Kamati hiyo itaongozwa na Mhariri wa Michezo wa gazeti Habari Leo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo ya Saccos ya Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Mgaya Kingoba na Katibu wa Kamati atakuwa Mhazini Mkuu wa Taswa, Shija Richard.

Wengine ni Mhazini Msaidizi wa Taswa, Zena Chande, mwandishi wa habari wa TBC1, Angela Msangi, Mwandishi wa habari wa gazeti la Majira, Masau Bwire na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Taswa, Chacha Maginga


CHANZO: Tanzania Daima   


No comments:

Post a Comment