Latest News

Tuesday, May 13, 2014

Tupa: Sililii safari, bali jina langu kutumika

Mwl. Samwel Tupa akitoa hoja
KOCHA maarufu wa riadha nchini, Samwel Tupa kutoka Arusha, amefafanua kwamba anacholilalamikia Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), ni jinsi jina lake lilivyotumika kama kocha aliyeondoka na wachezaji waliokwenda New Zealand kuweka kambi kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya Jumuiya ya Madola yanayotarajiwa kufanyika Julai mwaka huu, Glasgow Scotland.

Jina la kocha huyo lilitangazwa katika vyombo vya habari, kwamba ameondoka na wanariadha hao, lakini badala yake alikwenda Katibu Mkuu wa RT, Suleiman Nyambui, kama kocha wa wanariadha na yeye kuachwa bila taarifa.

Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu akiwa jijini Arusha, Tupa alisema anacholalamika yeye ni kwanini uongozi wa RT uliamua kutumia jina lake hadi dakika za mwisho, ilhali wamemuacha.

“Watu wanashindwa kuelewa, mimi silalamiki kuachwa katika hiyo safari, lakini kinachoniumiza mimi kwanini jina langu litangazwe kwamba naondoka wakati naachwa? Kwani kulikuwa na ulazima gani wa kutangaza jina langu, hilo ndilo swali langu?” aliuliza kocha huyo maarufu.

Alisema hajui waliotumia jina lake walitumia kwa malengo yapi, kwani hata uongozi wa RT wanapoulizwa kuhusu hilo, majibu yao yanagongana na yanatia shaka.

CHANZO: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment