Latest News

Wednesday, July 16, 2014

Kikwete ataka medali Jumuiya ya Madola

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, amewataka wachezaji wa michezo mbalimbali wanaokwenda leo kushiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola, kutambua heshima ya ushiriki wao na nchi pia. 
Kikwete aliyasema hayo jana wakati wa hafla ya kukabidhi timu hiyo bendera, iliyofanyika katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Aliwasihi wanamichezo hao kutambua kuwa ushiriki huo ni heshima kwao na taifa pia.

Alisema kuwa anaamini wakijituma wataweza kufanya vizuri na kurejea nchini wakiwa na medali badala ya visingizio vya maandalizi, kwa kuwa Wizara ya Mambo ya Nje chini ya Waziri Bernard Membe ilifanikisha suala zima la maandalizi kwa kuwapeleka nje ya nchi.

“Wachezaji kwanza mtambue heshima yenu kwanza kupata medali na taifa pia, kwani mimi na Watanzania wengine tuko nyuma yenu, msije mkashindwa mkasingizia maandalizi, mwaka huu yamefanyika,” alisema Kikwete aliyeambatana na Membe; Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Meck Sadik; Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia na wengine.

Kikwete alisema wakati mwingine wachezaji wanashindwa kwa woga tu na hofu, hivyo kuwataka waondoe hofu hiyo kwani ana imani watafanya vema katika michuano hiyo inayotarajia kuanza Julai 23 hadi Agosti 3 nchini Scotland.

Aliongeza kuwa Watanzania wanahitaji kufurahi kama Ujerumani walivyofurahi baada ya kutwaa Kombe la Dunia.
Katibu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi, aliishukuru Wizara ya Mambo ya Nje, na serikali kwa kutoa tiketi 11 za nyongeza kwa ajili ya wachezaji wengine na kusema mwaka huu wanaamini timu itafanya vema kutokana na maandalizi yaliyofanyika.

Rais wa TOC, Rashid Gulam, ameisihi serikali kutowachoka pale wanapoomba sapoti, kwani mwakani kuna michuano ya All African Games, huku pia akiwataka viongozi wengine kuiga mfano wa Waziri Membe kwani wakifanya hivyo, michezo itafika mbali.

Timu hiyo ya wachezaji 39, inaundwa na michezo ya riadha, kuogelea, baiskeli, judo, meza, ngumi za ridhaa na kunyanua vitu vizito.

Chanzo Tanzania Daima


No comments:

Post a Comment