Tufanye sensa ya vyama vya michezo nchini

Dioniz Malinzi / Bosi wa Baraza la Michezo Tanzania
Mwaka 2014 unakaribia kumalizika. Ni dhahiri hali ni mbaya katika medani ya michezo nchini na hiyo ni kutokana na matokeo tuliyoona kwa timu na wanamichezo wetu.
Kimsingi, Tanzania imeharibu na kutia aibu kuanzia soka, ambayo ndiyo mchezo maarufu, hadi michezo mingine.
Viongozi wenye dhamana katika michezo na wao wanaingiza siasa badala ya kuangalia nini wajibu wao na kwa chama na manufaa ya taifa. Tumewahi kupiga kelele sana katika eneo la michezo kuwa udhaifu wa uongozi na hasa kwa kutokuwa na dhamira na dira ya maendeleo, ndiyo kunachangia kutopiga hatua.
Kuvurunda kwa wanamichezo wa Tanzania katika mashindano mbalimbali, kutokana na kukosa umakini na zaidi ni udhaifu wa uongozi katika vyama na klabu. Kwa jinsi hiyo, itachukua muda mrefu Tanzania kupiga hatua katika michezo kama mfumo wa utendaji ndani ya vyama hautabadilika.
Kutokana na msingi huo, kuna haja kwa mamlaka inayohusika na michezo yote kufanya sensa ya vyama vya michezo ili kujua hadi sasa kuna vyama vingapi vilivyo hai na vina mahitaji gani. Mamlaka hizo ni Msajili wa Vyama vya Michezo, Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kurugenzi ya Michezo na juu zaidi ni wizara yenye dhamana na michezo.
Katika kufanikisha hili, iangaliwe, riadha wanafanya nini, nini programu yao ya mwaka? Je inatekelezwa? Nini matatizo na mafanikio, hivyo hivyo katika soka, netiboli, mpira wa mikono, wavu, ngumi, baiskeli, kikapu, kuogelea, skwashi na michezo mingine mingi. Kila mara tunasikia kuna uchaguzi katika vyama vya michezo, wanachagua viongozi, lakini je, ni kweli wanaoingia madarakani wana dhamira ya kweli ya kuendeleza mchezo husika?
Vyama hivi vyote ni vya kufanyia sensa ili kujua kama viko hai, vinaendeshwa kwa kufuata katiba, vyanzo vyao vya mapato ni nini, na vinahitaji msaada gani, na zaidi ya yote Serikali inawezaje kuvisaidia. Tuliona jinsi Serikali ilivyoshikia bango suala la mabadiliko ya katiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), na kudiriki hata kutaka kuvunja uongozi. Serikali inafanya nini kwa vyama vingine ambavyo havina hata katiba? havifanyi uchaguzi na wala havina hata utunzaji mzuri wa mapato yake?

Tunapata wasiwasi kwamba Serikali huingilia pale tu viongozi wake wanapokuwa na maslahi yao, na si kwa lengo la kuhakikisha vyama vinaendeshwa kidemokrasia.
Hivi sasa kuna chama kama Chama cha Wavu Tanzania, au mpira wa mikono, lakini havina mashindano kwa mwaka mzima. Havina hata ligi. Serikali haioni hilo?
Leo tuna wanamichezo wa kuogelea walioenda Scotland kwenye Michezo ya Madola. Hawa walipatikana vipi wakati hakuna mashindano ya kuogelea nchini? Serikali haina budi kuibuka na ikiwezekana kuangalia upya majukumu yake katika usimamizi wa vyama vya michezo na michezo kwa ujumla. Kama majukumu hayo yamepitwa na wakati, basi haina budi kujiangalia upya na kuyarekebisha ili yaende na wakati.
Mfumo wa siasa umebadilika sana tangu sheria iliyounda Baraza la Michezo ilipopitishwa na hivyo, lazima imepitwa na wakati sana. Kwa hiyo, kama Serikali itafanya sensa hiyo ya vyama, pia itathmini majukumu yake katika usimamizi wa michezo. Kauli hiyo ya maandalizi imekuwa ikitolewa kila mwaka, lakini hakuna jipya linalofanyika. Mambo ni yaleyale, viongozi wanashtuka dakika za mwisho kuandaa timu bila kujali ukubwa na umuhimu wa mashindano.
Maandalizi yanafanywa tu kama kielelezo kwamba yalikuwapo kabla ya timu au washiriki kwenda kushindana kushindana kimataifa, lakini siyo kwa lengo la kuhakikisha tunafanya vizuri. Ndiyo maana tunaona sensa itasaidia kujua vyama mfu na hai. Watanzania wanatamani kuona wanamichezo wake wanafika mbali katika kila hatua za mafanikio, lakini hawa walio na dhamana hawataki.
Wakati Michael Yombayomba alipotwaa medali ya Madola mwaka 1998 katika ngumi, alilakiwa kwa shangwe na nderemo za kutosha, ni kwamba Watanzania wanapenda mafanikio, Watanzania wana hamu ya mafanikio, lakini hawa waliopewa dhamana ni tatizo. Kimsingi, tunaona kuna haja ya kufanya sensa ya vyama vya michezo hai, viongozi ‘hai’, Katiba hai ili walau kuanza kufufua michezo Tanzania.

CHANZO: Mwananchi

Comments

Popular

GIDABUDAY KUHAMASISHA UJENZI WA KIJIJI CHA MICHEZO TANZANIA LENYE JINA YA MWANARIADHA MKONGWE BW.JOHN STEPHEN AKHWARI

Rio Olympics: Brazil win men's volleyball gold, GB's Joyce takes boxing silver – as it happened

Olympics 2016: Usain Bolt completes sprint double, Jade Jones retains taekwondo title

Rio Olympics: Swimmer Lochte apologises for 'robbery' saga