Latest News

Saturday, December 12, 2015

Wanahabari wanatarajia Rais Magufuli atawafuta machozi

Polisi wakimshambulia Mwakilishi wa Chanel Ten Mkoa wa Iringa, Daud Mwangosi Septemba 2 mwaka 2012. Picha ya Maktaba
Tangu Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli aingie madarakani Novemba 5, 2015 baada ya kuapishwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Watanzania wameridhishwa na hatua kadhaa zinazochukuliwa hususan katika kudhibiti mapato ya Serikali na kuhimiza uwajibikaji wa kizalendo.
Ni zaidi ya mwezi mmoja sasa tangu Serikali hii ambayo imeandika historia kwa kuwa na Makamu wa Rais mwanamke, Samia Suluhu Hassan. Viongozi hawa kwa kushirikiana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wamechukua hatua kadhaa zenye kutoa mwelekeo wa mwenendo wa Serikali ya Awamu ya Tano wakishirikiana na Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue.
Wameonyesha kuwa Serikali yao haitaki mzaha linapokuja suala la ukusanyaji wa mapato, matumizi ya fedha za umma na kikubwa kuondoa dhana kuwa utumishi wa umma ni sehemu ya watu kushibisha matumbo yao, ndugu zao na marafiki wao.
Hatua zilizochukuliwa;
Hatua zilizochukuliwa katika kipindi hiki ni pamoja na kuwekwa utaratibu mpya wa kudhibiti safari za nje ya nchi kwa maofisa wa Serikali na kwamba ofisa anayekusudia kusafiri nje ya nchi anatakiwa kwanza kupata kibali maalumu kutoka Ikulu.
Haikushangaza Makamu wa Rais, Samia alipopunguza wajumbe alioambatana nao katika safari yake ya kikazi nchini Afrika Kusini hivi karibuni. Licha ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuidhinisha msafara wa wajumbe 12 kuambatana naye, taarifa zinaeleza makamu huyo wa rais alipunguza idadi hiyo na kusafiri na wajumbe sita tu.
Siyo kwamba mkutano huo wa kilele baina ya China na Tanzania haukuwa na umuhimu mkubwa kwa masilahi ya Taifa, bali kutekeleza kwa vitendo dhana ya Serikali kubana matumizi na kuelekeza fedha nyingi kwenye miradi inayowanufaishaWatanzania wengi.
Rais Magufuli wakati anazindua Bunge la Kumi na Moja alisema, safari za maofisa wa Serikali nje ya nchi zimekuwa zikiligharimu Taifa kiasi kikubwa cha fedha kiasi cha kuathiri utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo.
Akitolea mfano alisema zaidi ya Sh365 bilioni zilitumika kugharimia safari za nje za watumishi wa Serikali mwaka wa fedha 2013/14 na 2014/15 pekee. Katika kipindi hiki uendeshaji wa mikutano, semina na warsha kwa Idara za Serikali zimewekewa utaratibu ambao utapunguza kwa kiasi kikubwa gharama na kuzuia matumizi makubwa kwenye hoteli za kifahari nchini au wakati mwingine hata nje ya nchi.
Tumeshuhudia pia sherehe za kitaifa na hafla za kupongezana zikiamriwa kufanywa kwa utaratibu mpya unaoondoa matumizi makubwa ya fedha za umma na badala yake kiasi kikubwa kinachookolewa huelekezwa kwenye huduma za kijamii au kufanikisha miradi ya maendeleo.
Kwa mshangao mkubwa, Watanzania wameshuhudia kuibuliwa kwa ukwepaji mkubwa wa kodi bandarini Dar es Salaam na zaidi ya makontena 2,400 yalipitishwa pasipo kulipiwa ushuru. Wengi wamebaki wameduwaa na kuhoji vipi suala hilo limewezekana? Intelijensia yetu ilishindwa vipi kubaini madudu haya?
Sakata la makontena limeendelea kuziweka kwenye msukosuko mkubwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzana (TPA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hadi sasa watumishi kadhaa wa ngazi za juu wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa polisi.
Katika mwendelezo huo watumishi kadhaa wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi. Rais aliamua pia kuvunja Bodi ya TPA na kumsimamishwa kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi kwa kushindwa kuisimamia TRA na TRL.
Kwa kifupi, Serikali ya Rais Magufuli imeonyesha dhamira ya kufanya mabadiliko na mapinduzi yenye lengo la kuthamini na kukuza usawa wa binadamu na kupunguza pengo la walionacho na wasionacho katika jamii ya Kitanzania.
Imedhamiria kujenga Taifa la wawajibikaji na si la watu kuishi kwa ujanjaujanja. Taifa ambalo mtu ataheshimika kwa namna anavyowatumikia wengine. Taifa ambalo wananchi wake wataona fahari kulipa kodi ili kuchangia maendeleo ya nchi yao.
Matarajio ya waandishi wa habari;
Ni katika muktadha huohuo, waandishi wa habari wanategemea kuona zama mpya zikifunguliwa kati yao na Idara za Serikali na kuondokana na sintofahamu zilizowahi kujitokeza huko nyuma ili kuongeza uhuru wa habari wenye kuchangia maendeleo ya taifa.
Wanahabari wa Tanzania wanahitaji kuona Sheria mpya za kusimamia shughuli zao za kila siku zikitoa uhuru zaidi na haki zaidi kuliko ilivyo sasa kama ambavyo tume kadhaa zilivyowahi kubainisha huko nyuma kuwa zilikuwa sheria kandamizi.
Wanatamani kuona mchakato wa kupitisha Miswada ya Sheria za Vyombo vya Habari wa 2015 na Muswada wa Sheria ya Habari wa mwaka 2015 ukishirikisha wadau wa habari ili kuwapa nafasi ya kuisoma na kupendekeza mambo wanayoona yana tija kwa ustawi wa sekta hiyo nchini.
Wadau wa habari hawatarajii kuona miswada hii ikiwasilishwa bungeni kwa hati ya dharura kama ilivyokuwa Machi mwaka huu Serikali iliipeleka bungeni kwa hati hiyo na kukumbana na upinzani mkali kutoka kwa wadau walioamua kupiga kambi mjini Dodoma.
Ni imani yangu kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inatambua kuwa sekta ya habari ni mdau muhimu katika ujenzi wa demokrasia, upanuaji na ukuzaji wa utawala bora, kuwapo kwa uwazi na ustawishaji wa utawala wa sheria nchini. Hivyo, haina budi kuwekewa mazingira rafiki na bora ya utendaji kazi.
Wadau wa habari wanategemea msukumo wa Serikali ya Awamu ya Tano katika kufanikisha upatikanaji wa sheria bora za habari na kuondokana na sheria kandamizi zinazotoa haki kwa vyombo vya habari kwa mkono wa kulia na kuzipora haki hizo kwa mkono wa kushoto.
Licha ya utawala Serikali ya awamu ya nne kufanya makubwa katika kuruhusu na kushamirisha uhuru wa wananchi kujieleza, zipo kumbukumbu za mambo ambayo yameitia doa awamu hiyo ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete. Wadau wasingependa kurejea kwenye zama hizo katika utawala huu wa Dk Magufuli.
Haya yasitokee tena
Wadau wa habari wasingependa kuona mauaji ya waandishi wa habari yakitokea wakati wakitekeleza majukumu yao halali kama ilivyotokea kwa mwandishi wa habari wa kituo cha runinga cha Channel Ten, mkoani Iringa, Daud Mwangosi.
Mwangosi aliuawa na polisi Septemba 2, 2012 katika Kijiji cha Nyololo Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa. Ni mauaji ya kinyama ambayo yameitia doa Serikali ya awamu ya nne na kwamba wanahabari hawako tayari kuona mauaji ya namna hiyo yanatokea tena nchini.
Wanatarajia kuona kazi halali ya kila mtu inatambuliwa, inaheshimiwa na kuthaminiwa kwa kuwa Serikali iliyopo madarakani sasa inahamasisha Watanzania kufanya kazi na si vinginevyo. Hivyo, ni aibu mtu kuuawa na chombo kilichoapa kulinda raia na mali zao tena wakati akitekeleza wajibu wake halali wa kikatiba.
Awamu ya Tano inatarajiwa kutoa matumaini mapya kwa wanahabari na kuwaondolea madhila na mateso kama aliyokumbana nayo aliyekuwa Mhariri Mkuu Mtendaji wa New Habari, Absalom Kibanda.
Kibanda alivamiwa usiku wa Machi 6, 2013, akapigwa, akaumizwa jicho, kucha, akakatwa kidole na kung’olewa meno. Aliachwa afe nje ya lango la nyumba yake iliyoko Mtaa wa Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.
Katika mfululizo wa matukio hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Hali Halisi Publications, Saed Kubenea ambaye sasa ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya Chadema, alimwagiwa tindikali machoni baada ya ofisi zao kuvamiwa mwaka 2008.
Kama matukio hayo hayakutosha, maiti ya mwandishi, Issa Ngumba wa Redio Kwizera iliokotwa katika pori la Mlima Kajuruheta, Kijiji cha Mhange, wilayani Kakonko mkoani Kigoma, mwaka 2013 baada ya kutoweka nyumbani kwake kwa siku tatu.
Matukio yaliyochukua roho za waandishi wa habari katika kipindi hicho yaliambatana na mengine mengi ya vitisho. Yapo ambayo wahusika waliyaripoti kwenye vyombo vya ulinzi na usalama na mengine hayajaripotiwa kutokana na sababu mbalimbali.
Wadau wa habari wanaamini kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itawaondolea sintofahamu hiyo, itaendeleza ushirikiano na vyombo vya habari ili viendelee kuisaidia Serikali katika kuibua ‘madudu’ yanayofanywa na watumishi wasio waaminifu wanaoshirikiana na watu wengine kutoka ndani na nje ya nchi kuhujumu harakati zetu za kujiletea maendeleo.
Waandishi kwa upande wao, wanatakiwa kuongeza weledi, kuzingatia sheria za nchi ili kutokuwa chanzo cha kuvurugika kwa uhusiano mzuri ambayo yamedumu kwa muda mrefu licha ya kukumbana na changamoto nyingi katika Serikali iliyopita.
Katika nchi inayoheshimu utawala wa sheria ni vema mtu, taasisi, chama cha siasa au chombo chochote cha Serikali kinapohisi au kujiridhisha kuwa hakikutendewa haki na mwandishi au chombo fulani kufuata taratibu zilizowekwa ili kupata haki na si vinginevyo.
Kila kada inastahili kujengewa mazingira stahiki ya kutimiza wajibu wake ili kuakisi dhana ya uwajibikaji inayojengwa na Serikali ya Rais Magufuli. Ni wakati wa nchi yetu kujenga utamaduni mpya kuheshimiana na kupeana ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya kikazi.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment