Latest News

Saturday, September 17, 2016

Wadau wanavyosaka dawa michezo kuporomoka

Waziri Nape Nnauye alifungua rasmi kongamano hilo jana - Kibaha
KWA miaka mingi Tanzania imekuwa ikifanya vibaya katika michezo mbalimbali kimataifa na kuifanya kutowika tena licha ya huko nyuma kung’ara. Kuanzia soka, riadha, ngumi, baiskeli, netiboli, mpira wa mikono na michezo mingine kibao, huko nyuma ilikuwa ikifanya vizuri, lakini sasa hakuna kitu.

Kutokana na kuchemsha huko katika michezo mbalimbali, Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) kwa siku mbili (jana na leo), imeamua kuendesha kongamano la kujadili michezo kutafuta dawa ya gonjwa hilo.
Kongamano la Michezo Kongamano hilo la aina yake ambalo linamalizika leo katika shule za Filbert Bayi, Mkuza Kibaha, mkoani Pwani kwa siku mbili linajadili matatizo na nini kifanyike ili kuirejesha Tanzania katika mafanikio ya huko nyuma, ambako ilifanya vizuri katika michezo.

Mara nyingi timu zetu zinaposhiriki mashindano ya kimataifa na kurudi nyumbani mikono mitupu, wadau wengi wamekuwa wakizinyooshea vidole bila ya kutoa suluhisho la nini kifanyike ili kufanya vizuri.
Kila mtu amekuwa akilaumu hata yule ambaye hana mchango wowote katika maendeleo ya michezo hapa nchini au kutosaidia kuchangia chochote katika michezo, lakini ndio huwa wa kwanza kuchonga.

Wadau pia wamekuwa wakilaumu wachezaji, vyama au mashirikisho ya mchezo husika, TOC, Baraza la Michezo Tanzania (BMT) pamoja na wizara inayohusika na michezo pale timu zetu zinapochemsha katika michezo ya kimataifa wakati majirani zetu wakifanya vizuri.

Maeneo muhimu sana Baadhi ya vitu ambavyo jana na leo vilikuwa vikijadiliwa na baadaye kupatiwa ufumbuzi ni pamoja na sababu za kuanguka kwa michezo nchini na nini kifanyike ili kuliondoa hilo. Umuhimu wa kuwepo kwa sera ya taifa ya michezo, jukumu la Serikali katika kusaidia na kuhamasisha michezo na ujengwaji wa kituo cha michezo.

Kuifanya michezo kuvutia zaidi wanawake na kuwa sehemu salama kwa jinsi hiyo. Umuhimu wa vituo vya mazoezi na michezo, vyuo vya michezo na maendeleo ya michezo hapa nchini kwa ujumla.
Kuangalia fursa za kibiashara katika michezo, hasa kuangalia jinsi sekta binafsi na zile za umma zinavyoweza kusaidia michezo kwa njia moja au nyingine. Sababu kuporomoka michezo Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi anasema kuwa lengo na kongamano hilo ni kujadili tulikotoka, tuliko na tunakokwenda katika michezo.

Tathmini ya Kamati ya Olimpiki Tanzania ni kwamba baadhi ya Vyama/Mashirikisho ya michezo baadhi yao sio hai kwa maana ya:- Kutofanya uchaguzi kwa muda mrefu kwa kuzingatia Katiba zao, kutokuwa na viongozi halali, kutofanya au kuandaa Mashindano ya Kitaifa au kushiriki Kimataifa.

Sababu nyingine ni kutolipa ada ya Chama/Shiriisho lao la Bara na Dunia. Mafanikio ya nyuma Tanzania ilifanya vizuri katika Michezo ya Olimpiki iliyofanyika Moscow, Urusi mwaka 1980 wakati Filbert Bayi na Suleiman Nyambui walipomaliza katika nafasi ya tatu katika mbio za meta 3,000 kuruka viunzi na maji na meta 5,000. Mbali na Olimpiki, Tanzania pia ilivuma sana katika Michezo ya Jumuiya ya Madola kwa kutwaa medali hadi za dhahabu katika michezo ya riadha na ngumi.

Na wanariadha kama akina Juma Ikangaa pamoja na kutotwaa medali katika Michezo ya Olimpiki, lakini alifanya vizuri mara mbili kwa kumaliza mbio za marathon ndani ya 10 bora, Mfano mwaka 1984 wakati wa Michezo ya Olimpiki iliyofanyika Los Angeles, Marekani Ikangaa alimaliza katika nafasi ya sita.

Mwaka 1988 Ikangaa alishiriki Michezo ya Olimpiki iliyofanyika Seoul, Korea ya Kusini na kumaliza katika nafasi ya saba. Tangu wakati huo hadi mwaka huu katika Michezo ya Olimpiki ya Rio 2016, Brazil, Alphonce Simbu aliweza kumaliza wa tano katika marathon.

Timu ya taifa ya soka, Taifa Stars, nayo iliwika katika soka la Afrika baada ya kufuzu katika fainali za mwaka 1980 zilipochezwa jijini Lagos, Nigeria. Lakini miaka ilivyozidi kwenda ndio nchi yetu imezidi kuporomoka kimichezo badala ya kupanda.

Source: Habarileo

No comments:

Post a Comment