Latest News

Tuesday, May 13, 2014

HATARI: Malinzi mfukuze Nyambui RT

Ni Jumatatu nyingine tena tunakutana wadau wa Uwanja wa Kuchonga, kama kawaida tukipeana changamoto za kispoti ili kuchochea ufanisi katika sekta hii muhimu katika jamii.

Bila shaka mu wazima wa afya na mnaendelea na majukumu ya ujenzi wa taifa kama kawaida, ila kwa wale ambao hali zao si shwari kwa namna moja ama nyingine, tunawaombea nafuu ya mapema.

Kama ada, kwa manufaa ya wale ambao hatukuwa nao wiki iliyopita, tupeane dondoo japo kwa ufupi kile kilichojiri Jumatatu iliyopita. Wiki iliyopita tuliangalia sakata la usajili wa aliyekuwa kiungo wa Yanga, Frank Domayo, ambaye alinyakuliwa na mabingwa wa soka Tanzania Bara, Azam FC, tukio lililowagusa mashabiki na wadau wengi wa soka hapa nchini.

Lakini tulichokizungumzia, si kusajiliwa kwake Azam, bali jinsi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilivyojiingiza katika suala hilo kwa mgongo wa tukio hilo kufanyika kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars, kisha kuamua kumteua Wakili Wilson Ogunde, kwa kile kilichoitwa kuchunguza tukio hilo na kulishauri shirikisho hatua za kisheria na kikanuni juu ya hilo.

Kimsingi katika hilo, na namna TFF ilivyolibeba, hatukuwaunga mkono, kwani kwanza hawakuainisha tatizo hasa juu ya kilichotokea katika usajili huo, pia taratibu za kambi ya Stars zinajulikana, hivyo kama zimekiukwa, ni wazi kanuni za kambi zinaeleza nini kifanyike.

Katika hili, wazi tulibainisha kwamba hatuungi mkono hatua iliyofikiwa na TFF ya kuteua wakili, kisa tukio la usajili wa Domayo kufanyika kambi ya Stars, kwani hatuoni kipya ambacho atakuja nacho Wakili Ogunde katika hili, labda kama kuna kitu zaidi ya kile ambacho kimeelezwa kimetokea huko Tukuyu, Rungwe. Hivyo ngoja tusubiri miujiza atakayokuja nayo Wakili Ogunde.

Baada ya dondoo hizo, sasa turejee katika mada yetu ya leo. Sekta ya michezo hapa nchini imekuwa ikikumbwa na wimbi la kukosa ufanisi wa kutosha kwa takribani miaka kumi hivi sasa, jambo linalotoa mazao ya kutofanya vizuri kitaifa na kimataifa.

Kati ya michezo ambayo imekuwa kimbilio la Tanzania katika michezo ya kimataifa, hususan ile ya All Africa Games, Jumuiya ya Madola na Olimpiki ni riadha, ambapo Watanzania wengi huweka mawazo yao katika mchezo huo kufanya vizuri na kuitangaza Tanzania kama ilivyokuwa miaka ya 70 hadi 80 mwishoni.

Lakini wakati mamilioni ya Watanzania yakiwekeza mioyo yao katika michezo hiyo, tatizo linabaki kwa waliopewa dhamana ya kusimamia mchezo husika, ambao ni vyama ama mashirikisho ya michezo kitaifa, hususan kwa riadha ni Shirikisho la Riadha Tanzania (RT).

Ukiliangalia shirikisho hilo, kwa miaka ya hivi karibuni limekuwa na historia ya kukumbwa na matatizo yatokanayo na katiba, wakati likielekea katika masuala mazito hususan uchaguzi mkuu.

Ukiperuzi historia ya TAAA ambayo sasa ni RT, imewahi kukaa madarakani miaka tisa bila kufanya uchaguzi, huku ikishuhudiwa migogoro ya kila namna na viongozi wake wa juu kugawanyika vipande.

Lakini juhudi za serikali enzi hizo, chini ya waziri aliyekuwa na dhamana na michezo wakati huo, Muhammed Seif Khatib, Mkurugenzi wa michezo wakati huo, Henry Ramadhani, Katibu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), na Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo wakati huo, Leonard Thadeo, walifanya kazi ya ziada wakati huo miaka ya 2006, ikiwamo kupuuzwa na kukejeliwa na viongozi wa TAAA sasa RT, ikiwamo hata kupelekwa mahakamani, lakini mwisho wa siku uchaguzi ukafanyika jijini Mwanza na kuuweka madarakani uongozi chini ya Rais Francis John na Katibu Mkuu, Mujaya Suleiman Nyambui.

Uongozi wa RT chini ya John na Nyambui ukafikia kikomo kwa uchaguzi uliofanyika Mei 2012 mjini Morogoro, ambako wadau wa michezo walikuwa wamejawa na shauku kujionea mabadiliko makubwa katika mchezo huo.

Katika uchaguzi huo uliofanyika hoteli ya Deluxe mjini Morogoro, chini ya usimamizi wa Kamati ya Uchaguzi ya RT, Baraza la Michezo la Taifa (BMT), na wizara yenye dhamana na michezo chini ya Mkurugenzi wa michezo, Leonard Thadeo, hatimaye ulipatikana uongozi mpya, chini ya Rais Anthony Mtaka na Nyambui akirejea madarakani katika nafasi ya Katibu Mkuu.

Lakini katika kitu kilichostua siku hiyo mara baada ya uchaguzi, Mwenyekiti wa BMT, Dioniz Malinzi, licha ya kuonyesha furaha yake juu ya kufanikisha mchakato wa uchaguzi, aliwapongeza wajumbe wa mkutano mkuu wa RT, lakini akishindwa kuficha mshangao wake juu ya Nyambui kurejea katika nafasi hiyo ya ukatibu mkuu.

Malinzi akiwapongeza wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa RT, alisema: “Hongereni wajumbe kwa kazi yenu nzuri, lakini huyu Katibu wenu Nyambui, mimi nitamfukuza. Sijawahi kushuhudia katibu wa aina hii, ambaye anakuja kwenye mkutano mkuu mikono mitupu bila ajenda.”
Malinzi alisema hayo kwa uchungu uliochanganya na hasira huku akifafanua kuwa amewahi kuwa kiongozi katika nyanja mbalimbali ikiwamo vyama vya wafanyakazi na michezo, lakini hajawahi kumuona katibu wa aina ya Nyambui.

Kwa haraka na kama hauko karibu au ndani ya RT, unaweza usimuelewe Malinzi, lakini kwa yaliyowahi kutokea ndani ya RT kabla ya uchaguzi wa 2012 na yanayoendelea hivi sasa, najikuta Mzee wa Kuchonga nikihoji, Malinzi kwanini umechelewa au unachelewa kumfukuza Nyambui kama ulivyotoa tahadhari siku ile ya uchaguzi?

Najikuta nikikumbuka kauli hii ya Malinzi, nikiiangalia RT jinsi inavyoendeshwa, ambako kila kitu kinafanywa na Nyambui kana kwamba anaongoza familia yake.

RT, imekuwa ni kawaida kuendesha matukio makubwa kabisa ya kitaifa na kimataifa bila kushirikisha vikao vya Kamati ya Utendaji.

Nyambui anamaliza kila kitu mwenyewe na mbaya zaidi, ufanisi hakuna, badala yake anazua majanga kila kukicha na kukipa chama mtazamo hasi mbele ya jamii.

Kutokana na tabia au udhaifu wa Nyambui, kabla ya uchaguzi wa 2012, amekisababishia chama hasara zaidi ya sh milioni 11 akishirikiana na aliyekuwa mhasibu, tatizo ambalo hadi leo linashindwa kutafutiwa suluhu.
Mbali na hilo, baada ya uchaguzi wa 2012, Nyambui kwa uzembe kabisa, aliendesha mashindano ya taifa bila kuishirikisha Kamati ya Utendaji, jambo ambalo limekuwa endelevu hivi sasa, na kukisababishia chama janga la kudaiwa zaidi ya sh milioni 20, ambapo tayari kimeburuzwa Mahakama ya Wilaya Temeke, na kipo hatarini kuadhibiwa zaidi kwa kulipa zaidi ya hizo fedha inazodaiwa.

Kama haitoshi, hivi sasa timu ya riadha na nyingine zitakazoiwakilisha nchi katika michezo ya Jumuiya ya Madola, Glasgow, Scotland Julai mwaka huu, ziko nje ya nchi kwa mafunzo, lakini ni mchakato ambao hauna baraka za Kamati ya Utendaji ya RT na madudu yashaanza kuibuka kwa majina ya watu kutumika katika safari hiyo ilihali hawamo, huku sekretarieti nzima ikishindwa kutoa ufafanuzi juu ya hilo, kwa madai Nyambui ambaye yuko nje ya nchi ndiye anajua!

Hii ni hatari na aibu, na hapa ndipo naikumbuka kauli ya Malinzi aliyoutoa Morogoro. Kuna usemi, ndege wa rangi moja huruka pamoja, lakini ndani ya RT kuna chiriku na bundi, sijui kama kuna kuruka pamoja hapo.
Kimsingi, RT kuna uozo, Kamati ya Utendaji haijakutana karibu mwaka mzima! Lakini hakuna juhudi za wahusika kushtuka wala kupiga kelele na mambo yanazidi kwenda mrama.

Baba Malinzi, jahazi linazama, tatizo unalijua, kwanini hujatekeleza kauli yako? Mfukuze Nyambui, ndiye ‘kirusi’ cha ubabaishaji katika riadha Tanzania. Tunajua kuna masuala ya kikatiba, lakini Baraza lina namna ya kutia msukumo kuondoa majanga kama haya. Kila la heri, tukutane wiki ijayo.

CHANZO: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment