Wambura hatishiki pingamizi Simba

Mgombea urais wa klabu ya Simba, Michael Wambura, amesema hana hofu na watu wanaomtishia kumuwekea pingamizi ili asigombee nafasi hiyo kwenye uchaguzi utakaofanyika Juni 29 jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya wanachama wa klabu hiyo walidai klabuni hapo mwishoni mwa wiki kuwa watamuwekea pingamizi mgombea huyo kwa madai kuwa hana vigezo vya kuwania nafasi hiyo.


Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Wambura alisema hawezi kurudi nyuma katika dhamira yake ya kuwania uongozi Simba na kwamba wanaotaka kumpinga wafanye hivyo.

Alisema kuwa anawania uongozi kwa kuwa ana vigezo na sifa za kuwania hivyo wanaotaka kumpinga waandae hoja zao.


"Siwezi kusikiliza maneno ya watu... hao wanaotaka kunipinga wafanye hivyo lakini dhamira yangu ni kuwania uongozi ndani ya Simba ili nitoe mchango wangu na kuindeleza Simba," alisema Wambura ambaye amewahi kuenguliwa kugombea uongozi hatua tatu.


Wambura alienguliwa kwenye uchaguzi uliopita wa Simba kwa kosa la kufungua kesi mahakamani, akazuiwa kugombea TFF kwa madai ya kutokuwa muadilifu na alipigwa zengwe pia katika uchaguzi wa chama cha soka cha Mara ndani ya miaka minne iliyopita.


"Sitishwi na maneno ya watu" alisema Wambura.
Wambura alisema wakati wa kupiga kampeni ukifika ataweka wazi malengo yake na sababu ya kuwania uongozi Simba.


Mbali na Wambura, mgombea wa nafasi ya makamu wa rais wa klabu hiyo, Jamhuri Kiwhelu 'Julio' alisema atawawekea pingamizi wanachama wanaowania uongozi ambao wapo kwenye uongozi unaomaliza muda wake chini ya mwenyekiti Ismail Aden Rage.


Viongozi hao ni pamoja na Swed Nkwabi na Joseph Itang’are wanaowania Makamu wa Rais, Said Pamba na Ibrahim Masoud wanaowania ujumbe.


Kwa upande wake, Nkwabi aliiambia Nipashe kuwa kama kuna mwanachama anataka kumuwekea pingamizi hana hofu na hilo kwa kuwa ni haki ya mwanachama yoyote na watashindana kwa hoja.


Alisema endapo watakaomuwekea pingamizi watashinda, hatakuwa na kinyongo.


Hata hivyo Nkwabi alisema anawania uongozi Simba kwa lengo la kuisaidia timu.


Simba inatarajia kufanya uchaguzi Juni 29 ambapo mpaka sasa watu 41 wameshachukua na kurudisha fomu za kuomba kuwania uongozi.


Endapo wagombea wote watapita, mchuano mkali utakuwa kwenye nafasi mbili za juu ambapo Wambura atachuana na Evans Aveva huku katika nafasi ya makamu wa rais mchuano utakuwa kati ya Julio, Nkwabi, Geofrey Nyange na Itang'are (Mzee Kinesi). 


CHANZO: NIPASHE

Comments

Popular

GIDABUDAY KUHAMASISHA UJENZI WA KIJIJI CHA MICHEZO TANZANIA LENYE JINA YA MWANARIADHA MKONGWE BW.JOHN STEPHEN AKHWARI

Rio Olympics: Brazil win men's volleyball gold, GB's Joyce takes boxing silver – as it happened

Olympics 2016: Usain Bolt completes sprint double, Jade Jones retains taekwondo title

Rio Olympics: Swimmer Lochte apologises for 'robbery' saga