Yaliyojiri Sokoine Mini Marathon 2014



MWISHONI mwa wiki, Aprili 12 mwaka huu, macho na masikio ya Watanzania wengi yalielekea katika Kijiji cha Monduli Juu, kilichopo Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha, kufuatilia kumbukumbu za miaka 30 tangu kufariki kwa Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania, Edward Moringe Sokoine.

Maadhimisho hayo yaliyohudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete, yaliadhimishwa kwa matukio mengi ya kukumbukwa, lakini moja ya matukio yaliyotokea katika kumbukumbu hizo, ni msimu wa pili wa mbio za Sokoine Mini Marathon mwaka 2014.

Mbio hizo zilianza majira ya saa mbili asubuhi, ambapo pamoja na kuwepo kwa ushindani mkubwa, kulikuwa na matukio mengi yasiyo ya kawaida, likiwemo la wanariadha kulazimika kupisha magari.

WANARIADHA WANASA KWENYE TOPE

Zikiwa zimesalia takribani kilomita mbili mbio za kilomita 10 zimalizike, wanariadha walijikuta wakibadilishana baada ya njia kujaa matope huku kukiwa na mgari mengi yaliyokwama barabarani.
Tukio hilo lilibadili mwenendo mzima wa mbio, ambako mwanaridha aliyekuwa akiongoza mbio hizo kwa muda mrefu, Alfonce Felix kutoka klabu ya Holili (HYAC), alijikuta akishindwa kwenda na kasi yake ya awali, kitendo kilichompa nafasi mwanariadha mkongwe, Fabian Joseph kutumia uzoefu wake kumpita na kuongoza mbio hadi mwisho.

FABIAN JOSEPH NA JACKLINE SAKILU WASHINDA KILOMITA 10

Mwanariadha Fabian Joseph kutoka Arusha, ambaye ni bingwa wa zamani wa dunia km 21, alishinda mbio za km 10 upande wa wanaume akitumia dk. 34:28.04 akimpita mwanariadha chipukizi, Alphonce Felix ikiwa imesalia kilomita moja mbio hizo zimalizike.

Nafasi ya pili ilikwenda kwa Alphonce Felix kutoka klabu ya Holili, ambaye alitumia dk. 34:45.39 huku bingwa mtetezi, Dickson Marwa kutoka wa HYAC, akiridhika na nafasi ya tatu akitumia dk. 34:57.47.
Kwa upande wa wanawake, bingwa wa mbio za Kilimanjaro Marathon Km 21, Jackline Sakilu, kutoka klabu ya JWTZ Arusha, aliibuka mshindi akitumia dk. 40:01:26, huku nafasi ya pili ikienda kwa Nathalia Elisante wa Arusha dk. 40:51:27 na nafsi ya tatu ikaenda kwa Failuna Abdi wa Winning Spirit dk. 41:13:54.

VIJANA HOLILI WATAWALA KM 2

Tukio jingine lililojiri kwa upande wa michezo mwaka huu, ni kitendo cha wanariadha wasichana wachanga kutoka HYAC mjini Holili, mkoani Kilimanjaro kuteka mbio za kilomita 2.

Katika mbio hizo, mshindi wa kwanza alikuwa ni Adelina Audax, aliyewaongoza wasichana wenzake kutawala mbio hizo akifuatiwa na Neema Mathias na nafasi ya tatu ikienda kwa Lidiuna Godfrey.

MICHEZO MINGINE

Kulikuwa na michezo mbalimbali ukiacha riadha, ambapo mchezo wa jadi wa kurusha mkuki nao haukuachwa nyuma, huku kukiwa na mabadiliko makubwa.

Kati ya mabadiliko hayo, ni waandaaji wa mwaka huu kuandaa zawadi kwa ajili ya walemavu, tofauti na ilivyokuwa katika msimu wa kwanza wa mbio hizo.

Nyumba ya marehemu Sokoine iliyoko Monduli Juu, ilifurika viongozi mbalimbali ambao kwa pamoja, walijumuika na familia kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 30 ya kifo cha kiongozi huyo mzalendo na mwanaharakati wa kweli, Edward Moringe Sokoine.

CHANZO: Tanzania Daima

Comments

Popular

GIDABUDAY KUHAMASISHA UJENZI WA KIJIJI CHA MICHEZO TANZANIA LENYE JINA YA MWANARIADHA MKONGWE BW.JOHN STEPHEN AKHWARI

Rio Olympics: Brazil win men's volleyball gold, GB's Joyce takes boxing silver – as it happened

Olympics 2016: Usain Bolt completes sprint double, Jade Jones retains taekwondo title

Rio Olympics: Swimmer Lochte apologises for 'robbery' saga