Yaliyojiri Sokoine Mini Marathon 2014
MWISHONI mwa wiki, Aprili 12 mwaka
huu, macho na masikio ya Watanzania wengi yalielekea katika Kijiji cha Monduli
Juu, kilichopo Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha, kufuatilia kumbukumbu za miaka
30 tangu kufariki kwa Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania, Edward Moringe
Sokoine.
Maadhimisho hayo yaliyohudhuriwa na
viongozi wa ngazi za juu wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete, yaliadhimishwa kwa
matukio mengi ya kukumbukwa, lakini moja ya matukio yaliyotokea katika
kumbukumbu hizo, ni msimu wa pili wa mbio za Sokoine Mini Marathon mwaka 2014.
Mbio hizo zilianza majira ya saa
mbili asubuhi, ambapo pamoja na kuwepo kwa ushindani mkubwa, kulikuwa na
matukio mengi yasiyo ya kawaida, likiwemo la wanariadha kulazimika kupisha
magari.
WANARIADHA WANASA KWENYE TOPE
Zikiwa zimesalia takribani kilomita
mbili mbio za kilomita 10 zimalizike, wanariadha walijikuta wakibadilishana
baada ya njia kujaa matope huku kukiwa na mgari mengi yaliyokwama barabarani.
Tukio hilo lilibadili mwenendo mzima
wa mbio, ambako mwanaridha aliyekuwa akiongoza mbio hizo kwa muda mrefu,
Alfonce Felix kutoka klabu ya Holili (HYAC), alijikuta akishindwa kwenda na
kasi yake ya awali, kitendo kilichompa nafasi mwanariadha mkongwe, Fabian
Joseph kutumia uzoefu wake kumpita na kuongoza mbio hadi mwisho.
FABIAN JOSEPH NA JACKLINE SAKILU
WASHINDA KILOMITA 10
Mwanariadha Fabian Joseph kutoka
Arusha, ambaye ni bingwa wa zamani wa dunia km 21, alishinda mbio za km 10
upande wa wanaume akitumia dk. 34:28.04 akimpita mwanariadha chipukizi,
Alphonce Felix ikiwa imesalia kilomita moja mbio hizo zimalizike.
Nafasi ya pili ilikwenda kwa
Alphonce Felix kutoka klabu ya Holili, ambaye alitumia dk. 34:45.39 huku bingwa
mtetezi, Dickson Marwa kutoka wa HYAC, akiridhika na nafasi ya tatu akitumia
dk. 34:57.47.
Kwa upande wa wanawake, bingwa wa
mbio za Kilimanjaro Marathon Km 21, Jackline Sakilu, kutoka klabu ya JWTZ
Arusha, aliibuka mshindi akitumia dk. 40:01:26, huku nafasi ya pili ikienda kwa
Nathalia Elisante wa Arusha dk. 40:51:27 na nafsi ya tatu ikaenda kwa Failuna
Abdi wa Winning Spirit dk. 41:13:54.
VIJANA HOLILI WATAWALA KM 2
Tukio jingine lililojiri kwa upande
wa michezo mwaka huu, ni kitendo cha wanariadha wasichana wachanga kutoka HYAC
mjini Holili, mkoani Kilimanjaro kuteka mbio za kilomita 2.
Katika mbio hizo, mshindi wa kwanza
alikuwa ni Adelina Audax, aliyewaongoza wasichana wenzake kutawala mbio hizo
akifuatiwa na Neema Mathias na nafasi ya tatu ikienda kwa Lidiuna Godfrey.
MICHEZO MINGINE
Kulikuwa na michezo mbalimbali
ukiacha riadha, ambapo mchezo wa jadi wa kurusha mkuki nao haukuachwa nyuma,
huku kukiwa na mabadiliko makubwa.
Kati ya mabadiliko hayo, ni
waandaaji wa mwaka huu kuandaa zawadi kwa ajili ya walemavu, tofauti na
ilivyokuwa katika msimu wa kwanza wa mbio hizo.
Nyumba ya marehemu Sokoine iliyoko
Monduli Juu, ilifurika viongozi mbalimbali ambao kwa pamoja, walijumuika na
familia kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 30 ya kifo cha kiongozi huyo mzalendo
na mwanaharakati wa kweli, Edward Moringe Sokoine.
CHANZO: Tanzania Daima
Comments
Post a Comment