Mataifa 21 kushiriki Uhuru Maratho
Innocent Melleck/Katibu wa Kamati ya Uhuru Marathon |
WANARIADHA kutoka nchi 21
wanatarajiwa kushiriki mbio za Uhuru Marathon zinazotarajiwa kufanyika jijini
Dar es Salaam Desemba 8, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Kamati ya Uhuru Marathon, Innocent
Melleck, alisema kujitokeza kwa wanariadha kutoka mataifa mbalimbali kumeongeza
hamasa kubwa ya mbio hizo.
Melleck alisema wanariadha kutoka
mataifa hayo ndio wamejiandikisha hadi sasa na wanaamini wengi wataendelea
kujitokeza ili kufanikisha lengo lake.
Alizitaja nchi wanazotoka wanariadha
hao hadi sasa kuwa ni Tanzania, Uganda, Kenya, Afrika Kusini, Ethiopia, Angola,
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Malawi, Marekani, Ujerumani, Jamaica,
Urusi, China, Japan, Venezuela, Comoro, Nigeria, Italia, Canada, Madagascar na
Uturuki.
“Hii ni faraja kubwa kwetu, kwani
inaonyesha kwa kiwango kikubwa lengo letu la kupigania amani, umoja na
mshikamano miongoni mwetu linakubalika na watu wengi duniani,” alisema.
Aidha, Melleck alisema usajili bado
unaendelea kwa wale wanaotaka kushiriki, ambako fomu zitakazotolewa kwa
mshiriki wa kilomita 3 atalipa sh 100,000, kilomita 5 sh 2,000 na washiriki wa
kilomita 21 na 42 watalipia sh 6,000.
“Tunachukua nafasi hii pia kuziomba
kampuni au taasisi mbalimbali zinazotaka kudhamini mbio hizo zijitokeze na
kufanya hivyo, kwani nafasi bado ipo na tukumbuke bila amani hakuna chochote
kinachoweza kufanyika,” alisema.
Comments
Post a Comment