Mkutano wa Katiba RT waota mbawa
Suleiman Nyambui/Katibu RT |
MKUTANO mkuu wa kupitisha rasimu ya Katiba ya Shirikisho la Riadha Tanzania
(RT), uliokuwa ufanyike mjini Morogoro Novemba 30 umepigwa kalenda.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, Katibu
Mkuu wa RT, Suleiman Nyambui, alisema mkutano huo umeahirishwa hadi
utakapotangazwa tena baada ya kuingiliana na sherehe za ujio wa Kombe la Dunia
litakalowasili nchini Novemba 29.
Alisema tayari ameanza kuwatumia taarifa wajumbe mbalimbali wa mkutano huo
kupitia njia ya barua na mtandao ili kuhakikisha taarifa hizo zinawafikia kwa
wakati na kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza kwao.
“Viongozi wote watakuwepo katika sherehe hizo, hivyo kamati ya utendaji
imeona isogeze mbele mkutano ili kuwapa nafasi wajumbe wetu kulishuhudia kombe
hilo, na ninaamini taarifa zitamfikia kila mmoja na hakutakuwa na tatizo
lolote,” alisema Nyambui.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka wajumbe wa mkutano huo kuwa wavumilivu na
kujiandaa kwa ajili ya mkutano huo hadi itakapotangazwa tena siku
utakapofanyika.
Lakini wakati Nyambui akitoa taarifa hizo, baadhi ya wajumbe wa Kamati ya
Utendaji na viongozi wa vyama vya mikoa, wameelezea kukerwa na kitendo hicho,
kwani tayari walikwishaomba ruhusa kwa waajiri wao, na RT imechelewa kutoa
taarifa rasmi ya kuahirishwa.
“Kama wamekosa fedha wangetuambia tu mapema, lakini mara tunasikia fununu
kuwa tatizo sio fedha bali ziara ya Kombe la Dunia, hivi kweli hivi vitu
vinaingiliana kweli?” alihoji kiongozi mmoja kutoka Tabora.
SOURCE: Tanzania Daima
Comments
Post a Comment