Baraza la mawaziri joto nyuzi 100: Taarifa zinasema rais Kikwete jana alikutana na makamu wake Dr. Gharib Bilal Ikulu
Mh. Rais Dr.Jakaya Kikwete |
Tangu mawaziri wanne, Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na JKT), Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii) na Dk David Mathayo (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi) walipovuliwa nyadhifa zao ikiwa ni hatua ya kuwajibika kutokana na madhila yaliyowapata wananchi kutokana na Operesheni Tokomeza Ujangili, na kifo cha aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, kumekuwa kuna kila aina ya uvumi.
Hata hivyo, kitendawili kilichobakia ni siku gani hasa Rais Kikwete atakapotangaza mawaziri wapya kwani hata wasaidizi wake wamekuwa wakikwepa kuzungumzia suala hilo na kuwataka wananchi kuvuta subira.
Taarifa zilizofikia gazeti hili jana, zilieleza kuwa Rais Kikwete alikutana na Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal Ikulu kujadili uteuzi huo.
Utaratibu unaelekeza pale Rais anapofanya uteuzi wa mawaziri hushauriana na Makamu wake na Waziri Mkuu. Chanzo kimoja kilidokeza kuwa kikao baina ya viongozi hao wawili kitaifa kilianza jana mchana.
“Kaka nakueleza tu wakuu wamekutana na hivi sasa ninavyoongea na wewe wanaendelea kujadili suala hilo ila sina uhakika mabadiliko haya yatangazwa lini,” kilidokeza chanzo hicho.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema: “Wananchi watulie na kumpa nafasi Rais Kikwete kupanga safu yake ya mawaziri.
Siwezi kusema atatangaza lini kwa sababu siwezi kumpangia siku ya kutangaza baraza, nadhani tusibiri tu mpaka siku atakapotangaza ndipo tutajua.”
Aliongeza: “Najua watu wana shauku kubwa lakini wanatakiwa kutulia tu muda mwafaka ukifika, kila kitu kitawekwa wazi.”
Balozi Sefue alisema uteuzi huo ni mzito na unahitaji umakini na muda huku akigoma kutoa ufafanuzi baada ya kuulizwa kuhusu kufanyika kwa kikao kati ya Rais na Makamu wake.
Uteuzi huo unafanyika baada ya Desemba 20 mwaka jana Rais Kikwete kutengua uteuzi wa mawaziri hao kutokana uchunguzi uliofanywa na kamati ndogo ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyoongozwa na James Lembeli.
Ripoti ya Kamati Ndogo ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyoundwa kuchunguza Operesheni Tokomeza ndiyo iliwang’oa mawaziri hao baada ya kueleza athari zilisababishwa na wizara nne walizokuwa wakiziongoza.
Chanzo: Mwananchi
Comments
Post a Comment