International Tennis Federation (ITF) yaibeba tenisi ya Tanzania
Viongozi wa TTA wakiongea na waandishi |
Shirikisho la Tenisi la Kimataifa (ITF) limetoa nafasi moja ya upendeleo kwa
mchezaji wa Tanzania kushiriki kwenye mashindano ya Tenisi ya Afrika kwa vijana
chini ya miaka 18 yaliyopangwa kufanyika mapema Machi katika nchi mbili
tofauti.
Awali Tanzania ilipitisha wachezaji wanne waliofuzu kushiriki kwenye
mashindano hayo ambayo yatafanyika jijini Nairobi, Kenya kwa wachezaji wenye
umri chini ya miaka 16 na Cassablanca, Morocco kwa wachezaji chini ya miaka 18.
Kwa mujibu wa kocha wa timu ya taifa ya vijana, Kiango Kipingu, chama cha
Tenisi Tanzania (TTA) kimepewa nafasi nyingine moja kwenye michuano hiyo ambayo
ITF imesema itachagua yenyewe mchezaji huyo ambaye itamghariamia kwa kila kitu.
“Kutokana na motisha hiyo ya ITF sasa Tanzania itawakilishwa na wachezaji
watano ambao wanne kati yao walifikia viwango vya kushiriki mashindano ya
Afrika baada ya kufanya vizuri kwenye yale ya Afrika Mashariki na kati hivi
karibuni jijini Dar es Salaam,” alisema Kipingu.
Alisema wachezaji waliofikia viwango, watatu wako Nairobi ambako huko wameweka
kambi na watashiriki kwenye mashindano ya dunia ya vijana chini ya miaka 18
yanayoendelea kwa wiki tatu jijini humo ambayo yatakuwa sehemu ya maandalizi
yao.
“Tumaini Mishuko, Emmanuel Malya na Omary Sule wako Nairobi ambapo baada ya
mashindano ya dunia watakwenda Morocco kule watashiriki mashindano mengine
ambayo yatakuwa sehemu ya maandalizi yao,” alisema.
Comments
Post a Comment