KATIBA: Nyongeza ya posho yagonga mwamba
Bunge la Katiba |
Madai ya Wajumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba kutaka nyongeza ya posho ya vikao vya Bunge hilo yamegonga mwamba,
Mwananchi limebaini.
Habari kutoka ndani ya kamati iliyoundwa na Mwenyekiti wa Muda
wa Bunge la Katiba, Pandu Ameir Kificho ili kufuatilia madai hayo, zimedai kuwa
baada ya uchunguzi wa kina, wajumbe wa kamati hiyo hawakuona sababu ya
kupendekeza posho hizo kupandishwa.
Taarifa hizo zilidai kuwa wajumbe hao wamefikia uamuzi huo baada
ya kupitia viwango vya posho vinavyolipwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Serikali na Mashirika ya Umma.
Pia kamati hiyo ilichambua viwango vya posho walivyolipwa
wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na viwango vya posho ya kujikimu vya
Sh80, 000 kwa siku wanavyolipwa watumishi wa Serikali.
“Hili jambo linahitaji busara sana na kutazama mazingira
ya nchi pia, kwa hiyo wajumbe wale baada ya kuoanisha viwango vya posho vya
taasisi mbalimbali wameona Sh300,000 zinatosha,” alisema mmoja wa wajumbe
ambaye hakutaka jina lake kutajwa.
Mjumbe mwingine, ambaye pia hakutaka kutajwa, alisema kuwa
watakaa leo kukamilisha taarifa ya utafiti wao, kabla ya kuikabidhi kwa
Mwenyekiti Kificho.
Alisema pamoja na umuhimu wa kazi za mbunge, lakini isingekuwa
rahisi kuongeza posho katika mazingira ya sasa, ambapo wananchi wanalia hali
ngumu ya maisha.
Wajumbe hao walioteuliwa na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu,
Pandu Ameir Kificho ni William Lukuvi, Mohamed Abood Mohamed, Freeman
Mbowe, Paul Kimiti, Jenister Mhagama na Asha Bakari.
Awali, taarifa kutoka ndani ya Bunge zilidokeza kuwa wajumbe hao
walikuwa wakutane jana saa 9:00 alasiri ili kuandaa ripoti itakayopelekwa kwa
Kificho ikiwa imebeba ushauri kuwa kiwango cha sasa cha posho kinatosha.
Sh300,000 wanazolipwa wajumbe wa Bunge Maalamu la Katiba
zinajumuisha Sh80,000 kwa siku ambayo ni posho ya kujikimu na Sh220,000 kwa
siku kama posho maalumu ya kuhudhuria kikao.
Posho maalumu ya Sh220,000 inajumuisha posho ya dereva
inayopaswa iwe kati ya Sh40,000 na Sh45,000 kwa siku, usafiri wa ndani (mafuta
ama teksi), mawasiliano na matumizi mengine binafsi.
CHANZO: Mwananchi
Comments
Post a Comment