Kili Marathon yatangaza njia mpya
WAANDAAJI wa Kilimanjaro Marathon wametangaza njia mpya zitakazotumika mwaka
huu, ikiwa ni hatua nyingine muhimu katika mafanikio ya mbio hizo ambazo
zinaingia mwaka wa 12 tangu kuanzishwa.
Njia hizo mpya zimelenga kuboresha mwendo wa washiriki barabarani na
kuwafanya wafurahie zaidi mbio hizo zilizopangwa kufanyika Machi 2 mjini Moshi,
mkoani Kilimanjaro.
Akitangaza njia hizo mpya jana, John Addison, Mkurugenzi wa Wild Frontiers,
waandaaji wa mbio hizo, alisema wameanzisha njia mpya ili kuzuia msongamano wa
watu wakati wa mbio kutokana na kuongezeka idadi ya washiriki kila mwaka.
Addson alisema washiriki wa mbio ndefu za marathon km 42, nusu marathon km
21, mbio za walemavu na mbio za kujifurahisha za Vodacom 5km Fun Run, sasa
hawatapishana tena barabarani, bali kila njia itatiririka katika muelekeo
mmoja.
“Pia kutokana na mabadiliko haya, washiriki watakuwa wameepuka kilomita 3 za
mwinuko mkali kuelekea Chuo cha Mweka ambapo awali ndipo palikuwa mahali pa kugeuzia
washiriki wa mbio za full marathon na half marathon.
“Mbio za walemavu za Gapco ambazo zitakuwa na makundi mawili tu mwaka huu ya
kiti cha magurudumu (wheelchair), na baiskeli ya mikono (handcycle),
zimefupishwa kutoka half marathon na kuwa km 10 ili kutoa fursa kwa watu wengi
zaidi kushiriki, na njia sasa itapita eneo tambarare na lenye kivuli,” alisema.
Alisema mbio ndefu za Kilimanjaro Premium Lager 42 km marathon zitaanza saa
12.30 asubuhi kutokea uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika na Biashara (MUCCoBS),
na kupita barabara iendayo Dar es Salaam kwa kilomita kumi na kurudia geti la
Ushirika halafu zitakwenda kilomita 8 kuelekea Hospitali ya KCMC na kukata
kushoto hadi Barabara ya Lema (Lema Road).
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa nusu marathon zitaanza saa moja kamili
asubuhi kutokea MUCCoBS na kupandisha kaskazini kuelekea Hospitali ya KCMC kwa
kilomita 8 ambazo ni sawa na ongezeko la mwinuko wa futi 250 kutoka usawa wa
bahari, kisha zitapita Lema Road na kurudi uwanjani.
Mbio za walemavu za Gapco Disabled 10 km marathon zitaanzia uwanja wa
MUCCoBS na kufuata barabara ya Kilimanjaro hadi Lema Road na kugeuza.
Addison alisema Vodacom 5km Fun Run zitaanzia mzunguko wa YMCA upande wa
Barabara ya Arusha na zitakwenda hadi kwenye mnara wa saa na kupita Boma Road
kuelekea mzunguko wa Barabara ya Arusha na mzunguko wa YMCA tena na watapita
Uru Road na kuingia uwanjani kupitia geti la mashariki.
Executive Solutions ni waratibu wa mbio za Kilimanjaro Marathon 2014
wakishirikiana na Riadha Tanzania (RT), Chama cha Riadha Kilimanjaro na
Kilimanjaro Marathon Club huku zikidhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager
(wadhamini wakuu), Vodacom Tanzania, GAPCO, Simba Cement, KK Security, Keys
Hotel, TPC Sugar, TanzaniteOne, CMC Automobiles Ltd, RwandAir, FNB Tanzania,
UNFPA na Kilimanjaro Water.
CHANZO: Tanzania Daima
Comments
Post a Comment