MATOKEO: Mfumo mpya ‘ahueni’ kidato cha nne
Dr Kawambwa/Waziri Elimu |
Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), limetangaza Matokeo ya
Mtihani wa Taifa wa kidato cha nne wa 2013, huku ufaulu ukiongezeka kwa
asilimia 15.17.
Matokeo hayo ni ya kwanza tangu kuanza kutumika kwa mfumo mpya
wa upangaji ambao ulipanua wigo wa alama na madaraja, hivyo kutoa nafasi kubwa
zaidi kwa watahiniwa kufaulu.
Licha ya kuanza kutumika kwa mfumo huo, idadi ya waliofeli
imeendelea kuwa kubwa kwani watahiniwa 151,187 sawa na asilimia 42.91 wamepata
sifuri. Kati ya hao, wavulana ni 78,950 sawa na asilimia 41.54 na wasichana ni
72,237 sawa na asilimia 44.51.
Kadhalika matokeo hayo yameendelea kushuhudia baadhi ya
watahiniwa wakiandika matusi kwenye karatasi zao za majibu, huku wengine
wakichora vitu vya ajabu kwenye mitihani hiyo, huku wengine wakishindwa
kuandika chochote kwenye karatasi hizo.
Akitangaza matokeo hayo jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu
Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alisema waliofaulu mtihani huo ni 235,227
sawa na asilimia 58.25 ya 404,083 ya waliofanya mtihani huo, ikilinganishwa na
185,940 sawa na asilimia 43.08, waliofaulu 2012.
Dk Msonde alisema wasichana waliofaulu ni 90,064 sawa na
asilimia 55.49 na wavulana ni 111,088 sawa na asilimia 58.45.
Alisema watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani huo walikuwa ni
427,679 wasichana wakiwa ni 199,123 sawa na asilimia 46.56 na wavulana walikuwa
ni 228,556 sawa na asilimia 53.44. Kati yao watahiniwa wa shule ni 367,163 na
watahiniwa wa kujitegemea ni 60,516.
Dk Msonde alisema watahiniwa 23,596 ambao ni sawa na asilimia
5.52 ya waliojiandikisha, hawakufanya mtihani huo.
Comments
Post a Comment