RIADHA HARD TALK 2014: RT yabariki mjadala wa riadha Holili
SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT), limeimwagia sifa klabu ya Holili Youth
Athletics (HYAC) iliyoko Holili, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro kwa kuandaa
mjadala wa kujadili changamoto zinazokabili mchezo wa riadha nchini.
Mjadala huo utafanyika kesho katika ukumbi wa Moshi Club ulioko pembezoni
mwa mji wa Moshi, mkoani Kilimanjaro, ambapo zaidi ya wadau 100 wanatarajiwa
kushiriki.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu, Katibu Mkuu wa RT,
Suleiman Nyambui, alisema shirikisho lake limetoa baraka zote kwa klabu hiyo na
mjadala huo na kutoa wito kwa wanamichezo wenye nia njema na maendeleo ya
riadha kujitokeza kwa wingi kushiriki.
Nyambui, aliwataka wadau wa riadha waelewe kwamba mjadala huo haujaandaliwa
kwa ajili ya kusutana bali kuunganisha akili kuangalia mbinu za kutatua
changamoto zinazokabili michezo hapa nchini.
“Watanzania na wapenzi wa riadha waelewe kwamba mjadala huu utalenga
kujadili matatizo yetu kama taifa katika riadha na kuangalia mbele, tusifike
mahali tukaanza kutumia mjadala huo kama uwanja wa mapambano,” alisema Nyambui.
Wakati huo huo, Kampuni ya vinywaji baridi ya Bonite Bottlers, imetoa msaada
wa vinywaji kwa klabu hiyo vitakavyotumika wakati wa mjadala huo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Meneja Mauzo wa Bonite,
Christopher Loiruki, alisema kampuni yake itaendelea kuunga mkono jitihada zote
zinazofanyika kuinua michezo hapa nchini.
“Sisi kama wadau wa michezo kila mara tutakuwa mstari wa mbele kusaidia
jitihada za kuinua michezo hapa nchini, kwa muktadha huo leo tunatoa kreti za
soda na maji kwa ajili ya mjadala wenu,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Holili, Domician Rwezaura, alisema lengo la
kuandaa mjadala huo ni kukusanya maoni ya wadau wa mchezo huo kuhusu nini
kifanyike kuufufua na kuurudishia hadhi yake kama ilivyokuwa katika miaka ya
nyuma.
“Tumeamua kuandaa mjadala huu sio kujionyesha au kuomba msaada, lengo letu
ni kutafuta mawazo ya wadau wa riadha juu ya nini kifanyike kufufua mchezo wa
riadha Tanzania na kuirudisha kule ilikokuwa miaka ya 70,” alisema Rwezaura.
CHANZO: Tanzania Daima
Comments
Post a Comment