Simba, Mbeya City zavunja rekodi
PAMBANO la Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), kati ya wenyeji Mbeya City na Wekundu
wa Msimbazi, Simba lililopigwa juzi Uwanja wa Sokoine, limevunja rekodi ya
mapato baada ya kuingiza sh milioni 105.
Katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1, na kujaza melfu ya
mashabiki, tiketi 21,000 ziliuzwa na baada ya makato, kila timu iliondoka na sh
25,316,630.58.
Kwa mujibu wa msimamizi wa Kituo cha Mbeya, Lwitiko Mwamundela, mgawanyo
mwingine ni VAT sh 16,016,949.15, gharama za uwanja sh 12,872,702.57, gharama
za mchezo sh 7,723,621.52 na Bodi ya Ligi sh 7,723,621.52.
Mgawo mwingine ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) sh 3,861,810.75 na Chama
cha Soka Mkoa wa Mbeya (MREFA) sh 3,0003,630.58.
Msimamizi huyo aliongeza kuwa mapato hayo yamevunja rekodi ya mchezo wa
mazunguko wa kwanza kati ya Mbeya City na Yanga, ambao uliingiza sh milioni 100
zilizotokana na mauzo ya tiketi 20,000.
Hata hivyo, licha ya mchezo huo kuingiza kiasi hicho cha fedha, changamoto
ilikuwa ni uchache wa tiketi, ambao ulisababisha mamia ya mashabiki kukaa nje
ya uwanja na wengine kuparamia miti na majengo marefu yaliyo karibu na uwanja
kwa lengo la kushuhudia mchezo hadi ulipofika muda wa ‘fungilia mbwa’ ndipo
walipoingia.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Mbeya City, Juma Mwambusi, alisema
matokeo ya sare ya 1-1, ni moja chachu ya kujipanga kwa ajili ya mchezo
unaofuata dhidi ya Coastal Union utakaopigwa Mkwawani jijini Tanga.
Kocha huyo amewatoa hofu wadau na mashabiki wa timu kuwa ana imani mchezo
utakaofuata watafanya vema ili kujihakikishia mazingira mazuri na hatimaye
kubeba ubingwa.
Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic, alikisifu kiwango cha Mbeya City kutokana
na uwezo waliouonyesha.
Alisema mechi za mikoani zinakuwa ngumu tofauti na zinazofanyika Uwanja wa Taifa
kutokana na wachezaji kuuzoea uwanja mmoja.
“Hata hivyo, timu yangu imejitahidi kwa asilimia kubwa, lengo ilikuwa ni
kushinda, kutokana na kiwango walichoonyesha Mbeya City hii pointi moja
inatosha kuliko kutopata kabisa, kwani tulikuwa tuna nafasi nyingi za kushinda
hasa kipindi cha pili, lakini wachezaji hawajazitumia,” alisema.
CHANZO: Tanzania Daima
Comments
Post a Comment