Wanariadha mashuhuri kuchuana Kili Marathon
John Bayo/Mwingereza/Musa Ninga |
WANARIADHA mashuhuri wa Tanzania wanatarajiwa kupambana vilivyo ili kutwaa
medali na fedha katika mbio za Kilimanjaro Marathon 2014 zinazotarajiwa
kufanyika Machi 2 mjini Moshi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa mbio hizo, John Bayo, wanariadha maarufu wa
Tanzania, Andrew Sambu, John Leonard na Daudi Joseph ni miongoni mwa wanariadha
Watanzania watakaoshiriki katika mbio za Km 42 kwa wanaume.
Katika mbio za kilomita 42 kwa wanawake, watakuwepo Banuelia Brighton,
Fabiola William na Flora Yuda, ambao wanatarajiwa kutoa upinzani mkali kwa
wanariadha wengine Watanzania pamoja na wa kigeni.
Andrew Sambu ana rekodi ya kumaliza Korea Marathon kwa saa 2:09:52 mwaka
2004 na mshindi wa medali ya fedha kwenye Mashindano ya Riadha barani Afrika na
ameshiriki Olimpiki, wakati Banuelia Brighton akiwa ameshinda Kigali Peace
Marathon mwaka 2009 na kumaliza wa pili Kampala Marathon mwaka 2011.
Dickson Marwa, mshindi wa Ngorongoro Half Marathon 2013 ambako alimaliza wa
kwanza akitumia saa 1:4:49, Alphonce Felix pamoja na Ezekiel Jafari ni kati ya
wanariadha ambao wataiwakilisha Tanzania kwenye mbio za Km 21 kwa wanaume huku
kwa wanawake wakitarajiwa Mary Naali, Jacqueline Sakilu na Sarah Ramadhani.
Akiwa ametengeneza rekodi nyingi, Mary Naali ni kati ya wanariadha bora
nchini katika mbio za Km 21 maarufu kama Half Marathon. Alishinda Vienna
Marathon mwaka 2010 akitumia saa 1:12:16 na baada ya hapo akavunja rekodi
kwenye mbio za kilomita 25 za Arusha VIP Race mwaka 2011 akitumia saa 1:20:52
na kuvunja ile ya 1:22:18 iliyokuwa imewekwa na Josephine Deemay mwaka 2006.
Mei mwaka 2013 pia alishinda mbio ya Bucharest International Marathon huko
Romania akitumia saa 1:16:32.
Naali atashindana na Sarah Ramadhani ambaye ni bingwa mtetezi kutokana na
ushindi wake kwenye Kilimanjaro Marathon 2013 alipomaliza akitumia saa 1:13:05.
Pia katika mchuano huo, atakuwemo Jacqueline Sakilu, ambaye ni kati ya
wanariadha wanaotarajiwa kufanya makubwa baada ya kushinda mbio kadhaa za
kilomita 21, ikiwemo Uhuru Marathon 1:15:25 na Ngorongoro Run 1:16:50.
“Tuna furaha kuwa na kikosi madhubuti kwa wanaume na wanawake. Uwepo wa
wanariadha hawa wazoefu, naamini utaifanya mbio hii iwe ya kuvutia,” alisema
John Bayo ambaye pia ni kocha maarufu wa riadha.
“Wanariadha wetu wana viwango vya kimataifa. Baadhi ya wanariadha wa kiume
wameishakimbia chini ya muda wa saa 2:15:00 huku upande wa wanawake wakiwa
wamekimbia chini ya 2:40:00. Hii ni mbio ya kimataifa, ambapo mshindi anaweza
kuwa mtu yeyote kutoka taifa lolote, lakini kinachotupa nguvu ni hamasa
tunayoipata kutoka kwa wananchi, maana mbio inafanyika hapa nyumbani, hivyo
basi tuko tayari kwa changamoto hii,” alisema.
Naye Aggrey Marealle, Mkurugenzi Mkuu wa Executive Solutions, waratibu wa mbio
hizo, alithibitisha kwamba, timu ya wanariadha inayoandaliwa na Holili
Athletics Club, imekuwa katika maandalizi kwa miezi minane iliyopita na wako
tayari kupeperusha bendera ya Tanzania. Timu hiyo imepunguzwa kutoka wanariadha
20 hadi wanane bora, ambao wako kwenye maandalizi ya mwisho.
Kwa upande wake, John Addison, Mkurugenzi Mkuu wa Wild Frontiers ambao ndio
waandaaji wa mbio hizo, alisema, takriban washiriki 6,000 kutoka nchi zaidi ya
40 duniani wanatarajiwa kushiriki kwenye mbio za 12 za Kilimanjaro Marathon.
Kilimanjaro Marathon 2014 inaratibiwa na Executive Solutions kwa ushirikiano
na Riadha Tanzania (RT), Chama cha Riadha Mkoa wa Kilimanjaro na Kilimanjaro
Marathon Club zikidhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager (wadhamini wakuu),
Vodacom Tanzania, GAPCO, Simba Cement, KK Security, Keys Hotel, TPC Sugar,
TanzaniteOne, CMC Automobiles Ltd, RwandAir, FNB Tanzania, UNFPA na Kilimanjaro
Water.
CHANZO: Tanzania Daima
Comments
Post a Comment