Jackline Sakilu, nyota anayechipukia riadha JWTZ
JESHI la Wananchi
Tanzania (JWTZ), ni miongoni mwa taasisi ambazo kutokana na asili ya utendaji
wake, imekuwa ikishiriki katika michezo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Kuna madhumuni yanatoa
kipaumbele cha michezo jeshini. Baadhi yake ni kujenga na kukomaza afya ya
mwili, akili na maisha bora kwa mafisa na askari. Kujenga ukakamavu, nidhamu na
uwezo binafsi wa kujihami katika jamii na taifa kwa ujumla. Hali
kadhalika kujenga tabia ya ushirikiano, upendo, umoja na uzalendo miongoni mwa
wanajeshi wenyewe na jamii nzima.
Aidha, imechangia sana
katika kutambua, kubaini na kuendeleza vipaji kwa wanajeshi na wananchi kwa
ujumla, kuwapatia burudani na kuitangaza Tanzania kimataifa, pamoja na
kujenga uhusiano mzuri wa majeshi ya nchi rafiki, na mengine duniani.
Lakini pia kutekeleza
maazimio ya shirikisho la michezo ya majeshi duniani (CISM) ambayo ni
kutumia michezo kama zana ya kueneza amani duniani badala ya vita, hivyo
kuitekeleza kauli mbinu ya urafiki kupitia michezo na mwisho kulifanya jeshi
kuwa kitalu cha maendeleo ya michezo nchini.
Mchezo wa riadha ni
miongoni mwa michezo kadhaa inayopewa kipaumbele ndani ya JWTZ.
JWTZ, liliwahi kutoa
wanariadha nyota wa kitanzania kama Philbert Bayi, Juma Ikangaa na wengine
wengi katika miaka ya 1970.
Baada ya nyota hawa
kustaafu mchezo huo, imepita miaka kadhaa Tanzania haikupata nyota wa riadha
kama hao. Kuna baadhi ya wadau wa mchezo huo waliofikia hatua ya kusema
kuwa pengine mchezo huo unaelekea kupotea kabisa katika ramani ya taifa hili.
Hivi karibuni, JWTZ limevumbua
kipaji kingine kipya katika mchezo wa riadha.
Private Jackline Sakilu, mzaliwa wa mkoa wa Singida alianza
mchezo huu akiwa na umri mdogo kabisa wa miaka tisa hivi ikiwa ni ngazi ya
shule ya msingi, kata, kanda na hatimaye ngazi ya kitaifa (UMITASHUMTA). Jackline anasema kuwa, mara baada ya
kumaliza elimu yake ya msingi alichaguliwa kujiunga na klabu ya riadha
iliyopo mkoani Arusha kwa ajili ya kufanya mazoezi ya mchezo huo, nia ikiwa ni
kuendeleza kipaji chake.
Akiwa katika kambi hiyo,
kwa mara ya kwanza alifanikiwa kuiwakilisha nchi katika mashindano ya mbio za
nyika za Dunia yaliyofanyika Ufaransa na kushika nafasi ya 32 kidunia.
Hivi karibuni katika
kusherehekea miaka 52 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Alishika nafasi ya kwanza
katika Mashindano ya Uhuru Marathon katika mbio za kilomita 21.
Pia alikuwa mshindi wa
kwanza katika Marathon iliyoandaliwa na Dar Rotary Marathon kwa upande wa
wakimbiaji wa kike iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Octoba
2013. Baada ya hapo alishiriki katika mashindano ya Afrika
Mashariki nchini Uganda katika mbio za Mita 800 na kushika nafasi ya nne.
Mwaka 2005 alishika
nafasi ya kwanza kwenye mashindano ya Taifa ya Riadha Dodoma, katika mbio za
Mita 800 na 1500. Huo ukawa mwanzo wa mafanikio makubwa kwa Jackline.
Mwaka 2009 JWTZ
lilitangaza ajira kwa watanzania wenye vipaji vya mchezo wa riadha kujiunga na
jeshi ili kuendeleza vipaji vyao.
Taarifa hizo bila shaka
zilikuwa njema kwa Jackline, ambaye kwa wakati huo alikuwa na hamu ya
kuendeleza kipaji chake. Mwaka 2010 alihitimu mafunzo ya awali na kufanikiwa
kujiunga na JWTZ na baadaye akajiunga na timu teule ya jeshi ya mchezo huo.
Baadaye mwaka 2012,
Jackline aliliwakilisha JWTZ kwenye michezo ya Majeshi ya Dunia, (CISM)
iliyofanyika Rio de Janeiro, Brazil na kufanikiwa kushika nafasi ya nne katika
mbio za kilomita 800. Mwaka 2012, aliliwakilisha tena JWTZ katika michezo ya
Majeshi kwa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki huko Burundi. Alishika nafasi
ya tatu katika mbio za Nyika za Kilomita nane kwa upande wa wanawake.
Hivi karibuni, Jackline
alishiriki katika mashindano ya kimataifa ya riadha nchini Brazil, yakihusisha
nchi za Kenya, Ethiopia, Ujerumani, Italia, Tanzania na Brazil.
Katika mashindano hayo
ambayo yalishirikisha jumla ya washiriki 900, Jackline aliibuka na medali saba
za dhahabu na moja ya fedha.
Katika mashindano hayo,
Jackline amelipatia heshima kubwa JWTZ na taifa kwa ujumla, na kuacha gumzo
nchini Brazil baada ya kuvunja rekodi zake kadhaa katika mashindano hayo kwa
kukimbia mwendo wa kasi zaidi kuliko ule wa awali.
Katika mbio za kilomita
21 na kilomita 10, alitumia dakika 71 na sekunde 28, tofauti na awali
ambapo alitumia dakika 73 na sekunde 17. Mbio za kilomita 10 alitumia dakika 33
na sekunde 15, wakati awali alitumia dakika 34 na sekunde 4.
Jackline anasema pamoja
na kuzingatia mazoezi, mafanikio hayo ni kutokana na malezi bora ya kukuza
vipaji ndani ya JWTZ pamoja na kuzingatia maelekezo anayopata kutoka kwa kocha
wake aliyemtaja kuwa ni Sajini Shaban Hiki.
Aidha, mbali na mchezo wa
riadha, Raia Mwema lilitaka kujua ushiriki wa JWTZ katika michezo mingine,
jitihada zinazochukuliwa na jeshi hilo katika kukuza michezo mingine. Msemaji
wa Jeshi, Luteni Kanali Erick Komba amefafanua; “JWTZ limekuwa likishiriki katika
Michezo ya Kimashindano na michezo kwa wote.
“Michezo ya Kimashindano
huhusisha ushiriki wa wanajeshi katika michezo ya kimashindano kitaifa na
kimataifa. Ushiriki huu hufanywa na timu teule ya JWTZ katika mashindano
mbalimbali yanayosimamiwa na mashirikisho husika ya michezo nchini kama vile
TFF kwa Mpira wa Miguu na vyama vingine,”
Aidha, anaendelea kusema
kuwa, JWTZ pia hushiriki katika michezo inayoandaliwa na Baraza la Michezo ya
Majeshi Tanzania (BAMMATA). JWTZ pia linasimamia Kituo cha Kukuza na Kuendeleza
Vipaji katika Michezo cha Twalipo Camp Youth Sports Foundation.
Pamoja na JWTZ kushiriki
kikamilifu michezo ndani ya nchi, limeshiriki pia katika michezo mbalimbali
kimataifa, kama vile mashindano yanayoandaliwa na mashirikisho ya Michezo ya
Majeshi ya Dunia (CISM) ambapo mwaka huu Tanzania itakuwa mwenyeji wa
mashindano hayo ambayo huhusisha karibu michezo yote kulingana na hali ya
uchumi kwa nchi mwenyeji.
Anasema kuwa, kwa ujumla
michezo hii hulenga kustawisha na kudumisha utimamu wa mwili na viungo kwa
wanajeshi wote.
Ushiriki wa JWTZ katika
michezo ya kimashindano ulianza mara baada ya vita ya Kagera 1979/80, ambapo
ziliundwa timu za jeshi.
Hii ilifanyika kwa
michezo baina ya vikosi na vikosi na hivyo kuteua wachezaji wenye viwango
vya kitaifa na kimataifa na kuunda timu teule za Jeshi. Timu za kwanza zilikuwa
ni za mpira wa Kikapu na Pete.
Chanzo: Raia Mwema
Comments
Post a Comment