KIKATIBA YEYE NANI? Kibali ujenzi Yanga mwisho wa mwezi
Mzee Ibrahim Akilimali |
WAKATI
Wazee wa Klabu ya Yanga wakipiga mkwara wa kutaka ndani ya siku tano wawe
wamepewa kibali cha ujenzi makao makuu ya klabu yao Jangwani, Halmashauri ya
Ilala imesema jambo hilo litaanza kufanyiwa kazi mwishoni mwa mwezi huu.
Juzi, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi ya Yanga, Francis Kifukwe,
alilalamika kuwa, licha ya kutuma maombi muda mrefu Manispaa ya Ilala kuomba
kibali cha ujenzi pamoja na kuongezewa eneo, lakini wahusika wamekuwa kimya na
kibaya zaidi, waliwafukuza kwenye kikao cha juzi.
Wakati Kifukwe akilalamika juzi, jana Katibu wa Baraza la Wazee
wa Yanga, Ibrahim Akilimali, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam kwamba, wanampa siku tano Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa,
kuhakikisha wanatoa kibali kwa klabu hiyo kuanza ujenzi wa uwanja unaotarajiwa
kuitwa ‘Jangwani City’.
Akizungumza kwa mbwembwe, Akilimali alisema, wanatoa siku hizo
kuhakikisha Silaa anatoa kibali, bila hivyo watahakikisha wanamwaga mboga,
kwani ugali wameumwaga wao.
“Tunajua manispaa inatuwekea kauzibe, na sisi Yanga ni klabu
kubwa na inafahamika toka enzi za Karume, hivyo basi, manispaa inamwaga mboga
na sisi tutamwaga ugali endapo siku tano tulizozitoa zitakosa majibu,” alisema
Akilimali aliyejitapa kupewa ruhusa ya kuzungumza na waandishi wa habari baada
ya hivi karibuni kupigwa ‘stop’ na mwenyekiti wa klabu hiyo.
Aidha, Akilimali alisema, mbali na kumwaga mboga, wameazimia
kufanya maandamano, ambayo yatamlenga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mecky
Sadick, Silaa na Rais Jakaya Kikwete.
Wakati hali ikiwa hivyo, Manispaa ya Ilala imekiri kupokea
maombi ya kuomba kibali kutoka uongozi wa klabu ya Yanga juu ya kutaka
kuuboresha uwanja wa timu hiyo uliopo eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,
Ofisa Habari wa Halmashauri hiyo, Lucy Semindu, alisema kuwa kamati ya mipango
miji na mazingira ya halmashauri hiyo ilipokea maombi hayo.
Semindu alisema kuwa, kamati hiyo itaanza ukaguzi wa eneo hilo
mwishoni mwa mwezi huu ili kuhakikisha wanajiridhisha kabla ya kuanza kwa
ujenzi huo.
“Uongozi wa timu hiyo uliwasilisha maombi ya kuomba kibali cha
ujenzi kwa ajili ya uwanja huo, ambayo yamepokewa rasmi na kamati husika,
ambayo wiki ijayo itafanya ziara kukagua eneo hilo,” alisema.
Alisema kuwa baada ya kuridhika na ukaguzi huo, halmashauri hiyo
itatoa kibali hicho mwishoni mwa mwezi huu.
CHANZO: Tanzania Daima
Comments
Post a Comment