UTAIFA KWANZA: Holili yadhamini Sokoine Mini Marathon
KLABU ya Holili Youth Athletic Club (HYAC) ya mjini Holili, mkoani
Kilimanjaro, imejitosa kudhamini mbio za Sokoine Mini Marathon
zinazotarajiwa kufanyika Aprili 12, mwaka huu katika Kijiji cha Monduli
Juu, Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha.
Katika udhamini huo, HYAC imetoa sh milioni moja zitakazotumika kuchapisha namba (Bibs), 1,000 za utambulisho za wanariadha.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Mkurugenzi wa HYAC,
Domician Genandi, alisema kilichomsukuma kufanya hivyo ni moyo wa
uanamichezo na kuongeza kuwa, kwa mwaka huu wamedhamiria kuongeza nguvu
zote kuinua mchezo wa Riadha nchini.
“Nimeamua kusaidia nikiwa kama mdau, sababu lengo letu ni kuendeleza
michezo Tanzania, sisi wadau tunatakiwa tuwe na mtazamo wa ushindi kama
taifa na si ushindi wa klabu zetu binafsi tu, au wanariadha wetu tu,
HYAC tunatambua jitihada binafsi zinazofanywa na waandaaji kumuenzi
hayati Sokoine,” alisema Genandi.
Aidha, Genandi alisema kwa mwaka huu klabu yake inatarajiwa
kushirikisha wanariadha wengi zaidi, ambako lengo lake ni kuhakikisha
anaendeleza rekodi ya mwaka jana.
Kwa upande wake, Mratibu wa mbio hizo, Wilhelm Gidabuday alisema kwa
udhamini huo HYAC inakuwa klabu ya kwanza ya riadha hapa nchini
kudhamini mashindano yanayoandaliwa na wadau wengine wa riadha na
kuongeza kuwa, katika hilo wameonesha kweli kwamba wana nia nzuri ya kuendeleza michezo hapa nchini hasa riadha.
Comments
Post a Comment