Fabian Joseph, Jackline Sekilu mabingwa Sokoine Min Marathon 2014
BINGWA wa mbio za Edmund World Half
Marathon nchini Canada mwaka 2005, Fabian Joseph, na bingwa wa Kili Marathon
2014 kwa wanawake, Jackline Sekilu, wameibuka washindi wa Sokoine Min Marathon
2014, katika mashindano ya Kumbukumbu ya Miaka 30 ya kifo cha aliyekuwa Waziri
Mkuu wa Tanzania, hayati Edward Moringe Sokoine, yaliyofanyika jana mjini hapa.
Fabian aliibuka mshindi wa kwanza wa
mbio hizo za kilometa 10 kwa kutumia dakika 34:28:04 na kufuatiwa kwa karibu na
Alphonce Frank wa Shule ya Winning Spirit aliyetumia dakika 34:41:89 na nafasi
ya tatu ikiangukia kwa mwanariadha Dickson Marwa wa Holili, aliyetumia dakika
34:57:47.
Kwa kuibuka kidedea, Fabiani
amezawadiwa fedha taslimu shilingi 500,000, kombe, medali na cheti maalum,
wakati mshindi wa pili akipata shilingi 400,000, medali na cheti, huku mshindi
wa tatu akipata shilingi 300,000, medali na cheti.
Wanariadha wengine waliomaliza
katika kumi bora na timu zao kwenye mabano ni Gabriel Gerald (Wining Spirit),
Fabiani Nelson (CCP Moshi), Pascal Sarwat (Holili), Andrea Samba (Wining
Spirit), Nyangero Patrick (Arusha), Shanga Gitina (ACSC) na John Leonard
(Wining Spirit).
Kwa upande wa wanawake, Jackline
Sekilu alitumia dakika 40:01:26, wakati nafasi ya pili ikienda kwa Natalia
Elisante (40:51:27), Failuna Abdi (41:13:59) na kufuatiwa na bingwa wa zamani
wa Kili Marathon, Mary Naali aliyeshika nafasi ya nne na wa tano akimaliza
Selina Amos kutoka Zanzibar.
Kwa upande wa mbio za walemavu,
washindi wa kwanza hadi wa tatu walitoka Dar es Salaam ambao pia walikimbia
kilometa 10, ambapo nafasi ya kwanza ilikwenda kwa Wilbert Costantino, wa pili
Shukuru Halfani na wa tatu alikuwa ni Mathias Solo.
Mashindano mengine yaliyopamba
maadhimisho hayo ya Sokoine Day 2014 ni pamoja na kutupa mkuki na kuruka juu
(Long Jump) na washindi wa kurusha mkuki walikuwa ni Said Thomas aliyefuatiwa
na Samson Kaura na Julius Daniel alikuwa wa tatu.
Kwa upande wa kuruka juu, Michael
Gwandu alikuwa wa kwanza kwa kuruka meta 6.80, akifuatiwa na Michael Danford
aliyeruka mita 6.37 na Kalum Said alikuwa wa tatu kwa kuruka mita 5.27.
Mmoja wa wadhamini wa mbio hizo,
Lulu Lengele alisema kuwa mfuko wa PPF wameamua kudhamini sehemu ya mbio hizo
kwa kutoa zawadi zote walizopewa washindi na wataendelea kudhamini mbio hizo na
michezo mingine kama sehemu ya afya kwa wananchi.
Wadhamini wengine wa mbio hizo
walikuwa ni Kampuni ya Mega Trade kupitia kinywaji cha K-Vant Gin
iliyowakilishwa na Meneja Masoko wake Goodluck Kway, ambaye aliridhisha na
mashindano hayo na kuahidi kuendelea kuyafadhili kwa miaka ijayo.
Alipokuwa akikabidhi zawadi hizo,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, alisema kuwa huo ndio
uzalendo unaotakiwa katika kuwaenzi mashujaa kama Sokoine, hivyo kuwataka
Watanzania kutomlilia huku wakiacha kufuata mema aliyokuwa akitenda, pamoja na
kuendeleza aliyoyaacha.
CHANZO: Tanzania Daima
Comments
Post a Comment