Tupa: Sililii safari, bali jina langu kutumika
Mwl. Samwel Tupa akitoa hoja |
KOCHA maarufu wa
riadha nchini, Samwel Tupa kutoka Arusha, amefafanua kwamba
anacholilalamikia Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), ni jinsi jina lake
lilivyotumika kama kocha aliyeondoka na wachezaji waliokwenda New
Zealand kuweka kambi kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya Jumuiya ya
Madola yanayotarajiwa kufanyika Julai mwaka huu, Glasgow Scotland.
Jina
la kocha huyo lilitangazwa katika vyombo vya habari, kwamba ameondoka
na wanariadha hao, lakini badala yake alikwenda Katibu Mkuu wa RT,
Suleiman Nyambui, kama kocha wa wanariadha na yeye kuachwa bila taarifa.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu akiwa jijini Arusha, Tupa alisema anacholalamika yeye ni kwanini uongozi wa RT uliamua kutumia jina lake hadi dakika za mwisho, ilhali wamemuacha.
“Watu wanashindwa kuelewa, mimi silalamiki kuachwa katika hiyo safari, lakini kinachoniumiza mimi kwanini jina langu litangazwe kwamba naondoka wakati naachwa? Kwani kulikuwa na ulazima gani wa kutangaza jina langu, hilo ndilo swali langu?” aliuliza kocha huyo maarufu.
Alisema hajui waliotumia jina lake walitumia kwa malengo yapi, kwani hata uongozi wa RT wanapoulizwa kuhusu hilo, majibu yao yanagongana na yanatia shaka.
CHANZO: Tanzania Daima
Comments
Post a Comment