TOC yaigomea RT: Viwango na Vigezo kuzingatiwa

Mwanariadha mkongwe Tanzania Andrea Sambu Sipe (Pichani) na Musanduki Mohamed ndio pekee waliofikia viwango vinavyohitajika, kwa maelezo ya TOC hawawezi kuachwa maana viwango wanavyo.

Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) imelikataa ombi la Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) la kutumia mashindano ya taifa ya riadha kuteua timu itakayoshiriki kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola.

Mapema jana, Katibu Msaidizi wa RT, Ombeni Zavala aliiomba TOC kuvuta subira hadi watakapomaliza mashindano ya taifa yatakayoanza Julai 12 na 13 ili kujua hatima ya kikosi chao cha Madola.

“RT tunategemea kutumia mashindano ya taifa ili kupata timu itakayokwenda katika michuano ya Jumuiya ya Madola, hivyo tunaomba TOC itupe muda yatakapokwisha mashindano tutapeleka kwao kikosi kamili,” alisema Zavala.

Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi, alikataa ombi hilo na kusema kama RT inahitaji kuteua timu kwenye mashindano ya taifa waitumie kwenye mashindano mengine ya kimataifa na si Madola.

“Hatuwezi kuwasubiri RT hadi wamalize mashindano ya taifa ndipo wataje timu ya Madola, kama wanataka watumie mashindano hayo kutengeneza timu ya ‘All African Games’ na mashindano mengine lakini si haya,” alisema Bayi.

Alisema RT na vyama vingine vinavyopeleka wanamichezo kwenye mashindano ya Madola vilipaswa kupeleka taarifa za wanamichezo wao kabla ya Mei 30, na Juni 11 ndiyo itakuwa mwisho wa waandaaji nchini Scotland kuyapokea na baada ya hapo hakuna mchezaji atakayepokewa.

Kwa mujibu wa katibu huyo, kesho vyama vya michezo vilivyoteuliwa kuiwakilisha nchi Madola, Serikali na TOC vitakutana kwa ajili ya kuangalia waliofikia viwango vya kwenda kwenye michezo hiyo itakayoanza mwishoni mwa Julai jijini Glasgow.

“Naomba nieleweke, katika uteuzi wa wanamichezo tutaangalia viwango, si lazima walioko kwenye kambi nje ya nchi kwenda wote kwenye Madola hata kama hawajafikia viwango tulivyokubaliana,” alisema Bayi.

Tanzania imepewa nafasi 36 kwenye michezo ya riadha, ngumi, judo, mpira wa meza, kuogelea, paralimpiki, baiskeli na kunyanyua vitu vizito kushiriki kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola msimu huu, na wanamichezo wa michezo sita kati ya hiyo wako kwenye nchi za China, Uturuki, New Zealand na Ethiopia kwa maandalizi.

CHANZO: Mwananchi





Comments

Popular

GIDABUDAY KUHAMASISHA UJENZI WA KIJIJI CHA MICHEZO TANZANIA LENYE JINA YA MWANARIADHA MKONGWE BW.JOHN STEPHEN AKHWARI

Rio Olympics: Brazil win men's volleyball gold, GB's Joyce takes boxing silver – as it happened

Olympics 2016: Usain Bolt completes sprint double, Jade Jones retains taekwondo title

Rio Olympics: Swimmer Lochte apologises for 'robbery' saga