Glasgow: Emiliani anyukwa, Ikangaa, Bazil leo
Dar es Salaam. Bondia Emiliani Patrick ameendeleza rekodi mbaya
ya Tanzania kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola baada ya jana kupokea
kipigo kutoka kwa Mganda Bashir Nasir.
Bondia Emiliani Patrick aliaga kwenye michezo hiyo baada ya kuruhusu kipigo cha pointi za majaji 2-1 dhidi ya Mganda huyo.
Katika pambano hilo, Emiliani alipata matokeo ya
pointi 28-29 raundi ya kwanza, 27-30 na raundi ya mwisho aliongoza kwa
pointi 29-28.
Kwa matokeo hayo sasa mategemeo ya Tanzania walau kutwaa medali kwenye michezo hiyo yamesalia kwa wanamichezo watatu.
Hadi jana, wanamichezo 36 wa Tanzania walioshiriki
ngumi, riadha, judo, mpira wa meza, kunyanyua vitu vizito, kuogelea na
baiskeli walikuwa tayari wameondoshwa kwenye mashindano hayo.
Tegemeo pekee kwa Tanzania lipo kwa wanariadha,
Dotto Ikangaa na Bazil John watakaochuana katika mbio za kati za mita
1,500 na bondia, Hamad Furahisha aliyetarajiwa kuzichapa jana usiku.
Kwa mujibu wa meneja wa timu za Tanzania kwenye
michezo hiyo, Muharami Mchume, wanariadha Ikangaa na John watachuana
katika mchujo kutafuta tiketi ya kuingia fainali kwenye mbio hizo
zitakazofanyika kwenye Uwanja wa Hampden Park jijini Glasgow.
“Furahisha atazichapa na Paddy Barnes wa Ireland
Kaskazini jioni hii ‘jana’ kwenye ukumbi wa SECC 4A katika pambano la
uzani wa light fly akishinda anaingia robo fainali,” alisema
Juzi jioni kwenye Uwanja wa Hampden Park,
Watanzania, Fabian Sulle na Wilbaldo Malley walishindwa kufurukuta
katika fainali ya mbio za mita 5,000 na kushuhudia Caleb Ndiku wa Kenya
akiibuka kinara baada ya kukimbia kwa dakika 13:12:07.
Isiah Koech wa Kenya aliyekimbia kwa dakika
13:14:06 alimaliza wa pili huku Zane Robertson wa New Zealand
akihitimisha tatu bora baada ya kukimbia kwa dakika 13:16:52.
Katika mbio hizo zilizoshirikisha wanaraidha 24,
Sulle alimaliza kwenye nafasi ya 14 akiwa amekimbia kwa dakika 13: 44:65
na Malley alimaliza kwenye nafasi ya 18 akitumia dakika 14:10:92.
Kwenye ngumi, bondia Gaudence Pius ameshindwa
kutamba mbele ya Sean Duffy wa Ireland Kaskazini na kuruhusu kipigo cha
pointi za majaji 2-1 kwenye pambano lake la kutafuta tiketi ya kucheza
robo fainali kwenye ukumbi wa SECC 4A.
Jaji wa kwanza alimpa ushindi wa pointi 29-28 kwa Pius, jaji wa pili 28-29 na jaji wa tatu alimpa Pius pointi 28-29. Tanzania imetwaa medali sita za dhahabu, tisa za
fedha idadi sawa na medali za shaba katika Michezo ya Jumuiya Madola
tangu 1962.
Michezo mingine ya Tanzania inayoshindanishwa kwenye madola ni riadha, ngumi, baiskeli na kunyanyua vitu vizito.
CHANZO: Mwananchi
CHANZO: Mwananchi
Comments
Post a Comment