Nyambui: Niliomba nifungwe miaka 100 jela
Kocha wa timu ya taifa ya riadha na Katibu Mkuu wa Shirikisho la
Riadha Tanzania (RT), Suleiman Nyambui amesema aliomba afungwe miakba
100 jela kama ikibainika anajihusisha na usafirishaji wa dawa za
kulevya.
Kocha huyo mpya wa timu ya taifa alisema bado
anateswa na ‘mzimu’ wa kashfa ya kusafirisha dawa za kulevya iliyowahi
kumkabili, kashfa iliyoichanganya familia yake na yeye mwenyewe.
Nyambui aliliambia gazeti hili katika mahojiano
maalumu kuwa, katika maisha yake ya riadha tangu akikimbia miaka 1970
hadi hivi sasa akiwa ni kocha na katibu mkuu, hakuna changamoto kubwa
ambayo hataisahau kama siku alipoitwa kuhojiwa juu ya tuhuma hiyo.
Kigogo huyo wa RT alisema alijikuta akiingia
matatani na kuhojiwa na kitengo cha kudhibiti dawa za kulevya hapa
nchini kwa saa sita mfululizo juu ya kuhusika kwake na uuzaji na
usafirishaji wa dawa za kulevya.
“Kiukweli watu wa kitengo cha kudhibiti dawa za
kulevya walikuwa na vielelezo vyote vya namna RT ilivyohusika kuwaombea
visa watu waliokamatwa na dawa za kulevya ambao nakiri mimi ndiyo
nilihusika kuwaombea, lakini sikujua kama ni wauza ‘unga’,” alisema
Nyambui.
Watu hao walikuwa wadhamini wa RT na waliwasaidia
wanariadha wa Tanzania kwenda Australia kushiriki mashindano ya
kimataifa ya kutafuta viwango vya kushiriki Olimpiki ya 2008 huko
Beijing, China.
“Kiukweli sikujua kama wanahusika na kusafirisha
dawa za kulevya, hivyo hata waliposema wanakwenda kuipa sapoti timu huko
sikuona ajabu kwa kuwa walionekana kupenda riadha hivyo RT tukafanya
jitihada za kuwaombea Visa kwenye ubalozi wa Australia nchini Kenya,”
alisema Nyambui.
Inaendelea Uk.31
Alisema waliondoka wanariadha watatu na wadhamini
wao hao, lakini wakiwa uwanja wa ndege wa Australia, ujumbe huo wa
Tanzania ulihisiwa kubeba dawa za kulevya ndipo walikaguliwa na kukutwa
nazo.
“Nilipigiwa simu na askari wa Australia na ubalozi
wa Australia Kenya juu ya watu hao hata hivyo wanariadha niliowaombea
wakatufute viwango wao waliposachiwa hawakukutwa na dawa za kulevya
isipokuwa wale wadhamini ambao walikutwa nazo,” alisema Nyambui.
Anasema alipata misukosuko ya hapa na pale japo ushirikiano
alioutoa kwenye ubalozi na kitengo cha kudhibiti dawa za kulevya hapa
kwa kueleza ukweli ndivyo vilimuweka huru japo alitakiwa kuripoti kila
Ijumaa makao makuu ya kitengo hicho kwa mahojiano zaidi hadi pale
uchunguzi ulipopatikana.
“Siku ya kwanza nilipoitwa kwenye kitengo cha
kudhibiti dawa za kulevya hapa nchini nilihojiwa kwa saa sita, hali ile
iliniathiri na kuipa wakati mgumu familia yangu, nakumbuka kila baada ya
dakika 10 niliomba ruhusa kwenda kujisaidia kutokana na kiwewe, lakini
nasisitiza watu wale sikujua kama wanahusika na dawa za kulevya hivyo
walipokuja kutusaidia ukizingatia na hali halisi ya chama hatujiuliza
mara mbili, kama ‘ningetonywa’ mapema sidhani kama ningebeba msalaba
huo.”
Kwanini anang’ang’ania madaraka RT
Nyambui ambaye amekuwa akilalamikiwa kung’ang’ania
madaraka RT bila mafanikio alisema anaongoza riadha kwa mapenzi yake
kwa kuwa ni mchezo ulioko kwenye damu yake tofauti na wengi wanavyodhani
kuwa ana maslahi binafsi ndani ya shirikisho hilo.
“Kuna wakati uwa natamani kuacha kuongoza RT,
lakini nashindwa kwa kuwa riadha hiko kwenye damu yangu, japo nafanya
kazi katika mazingira magumu ila naamini katika maisha ya kawaida
binadamu wote hawawezi kukupenda wapo wanaotambua mchango wangu kwenye
riadha na wanaonichukia pia wapo.”
Fedha za IAAF zinatumikaje
“IAAF (Shirikisho la riadha la kimataifa) uwa
linaipa nchi wanachama kiasi flani cha fedha ambapo kwa Tanzania inapata
dola 15,000 kwa mwaka, fedha hizo ni kwa ajili ya shughuli mbalimbali
za riadha,”
Anasema IAAF inatoa fedha hizo baada ya chama cha
kitaifa kufanya aidha mashindano, kozi na vitu vingine vya riadha
ambavyo vinakifanya chama kuwa hai.
“Mfano tumefanya mashindano ya taifa hivyo
tukituma ripoti hiyo IAAF tunafuzu kupewa dola 5,000, tukifanya kitu
kingine kama kozi tunapewa fedha nyingine ambazo fedha hizo ni kwa ajili
ya mambo ya kiutawala, haturuhusiwi kutoa hata senti moja kwenye
mashindano ya taifa kwa kuwa IAAF inasema mashindano ya taifa na ya
kwetu wenyewe hivyo ikibainika tumetumia kwa ajili hiyo tunaweza
tukanyimwa kabisa.”
Kwa nini wanariadha wanagomea timu ya taifa
“Wanariadha wengi wa Tanzania hawana elimu ya
darasani, hili ni tatizo japo watu uwa wanaamini michezo ainahusiani na
elimu, lakini si kweli, elimu inaendana na michezo kama wangekuwa
wamesoma wangekuwa mbali.
“Wengi wanapelekwa pelekwa, mtu anafikiria fedha
za haraka haraka lakini anashindwa kutambua kama akiiletea nchi medali
anaweza kupata fedha zaidi ya zile anazopata kwenye mbio za fedha
wanazokimbilia na kukataa kujiunga na timu ya taifa,”.
Anasema wanariadha wa Tanzania wangeweza
kufanikiwa zaidi kupitia riadha kama wangekuwa na elimu kwani wanakosa
ofa za kimasomo nje ya nchi kama ilivyo kwa Wakenya na Waganda kwa kuwa
wengi wameishia darasa la saba na kidato cha nne.
Kupitia riadha alinunua nyumba Marekani
“Kupitia riadha nimefanikiwa kununua nyumba
Marekani huko Texas ambapo anaishi mtoto wangu wa kiume nilizaa na
mzungu, pia nimejenga Buzuruga na Bukumbi Misheni jijini Mwanza na hapa
Dar es Salaam mbali na riadha mimi ni mfanyabiashara wa maduka,”
alimaliza Nyambui.
CHANZO: Mwananchi
CHANZO: Mwananchi
Comments
Post a Comment