Riadha Taifa madudu, nyota wa Madola hoi

MASHINDANO ya taifa ya riadha yalianza jana katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku yakigubikwa na dosari nyingi, ikiwemo wanariadha watakaoshiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola kuchemka.

Kushindwa huko kumekuja ikiwa ni siku chache kabla ya timu ya Tanzania kuondoka nchini kwenda mjini Glasgow, Scotland kwa mashindanbo hayo yatakayoanza Julai 23 hadi Agosti 3.

Miongoni mwa dosari katika mbio za mwaka huu, ni maandalizi duni yaliyofanywa na Riadha Tanzania (RT) kwani baadhi ya wanariadha wameendelea kukimbia bila viatu kama mwaka jana.

Baadhi ya wanariadha jana walishiriki mbio hizo bila jezi rasmi, wengine wakivalia jezi za soka kwa mfano Kiabo Kahorwe kutoka Shinyanga.

Kahorwe alisema amefanya hivyo kwa kukosa fedha za kununua vifaa, hivyo kwa vile anaupenda mchezo huo, akaamua kujitafutia nauli tu ya kumpeleka Dar es Salaam na kurejea kwao.

Wengine walionekana wakishiriki wakiwa wametinga gauni, sketi na blauzi, huku baadhi yao wakiwa peku na wengine wakiishia kuvalia soksi bila vuatu kuashiria uduni wa kutisha.

Kwa RT hii chini ya Rais Anthony Mtaka, si mara ya kwanza kwa mbio hizo kufanyika katika mazingira duni kwa kiwango hicho japo mwaka jana, uongozi ulijitetea kuwa ni hali ya kawaida.

Dosari nyingine katika mbio hizo, ni kufanyika bila kufunguliwa rasmi kama ilivyo kwa mashindano mengine ya kitaifa katika kuonyesha uzito na mantiki ya mashindano yenye sura ya kitaifa. Mashindano hayo yalifunguliwa kwa mbio za mita 10,000 huku Dickson Marwa kutoka Mkoa wa Mara, aliibuka kidedea akitumia muda wa dakika 28:30.22. 

Madola hoi: Katika hali isiyotarajiwa, wanariadha walioweka kambi nje ya nchi kujiandaa na mashindano ya Jumuiya ya Madola mjini Glasgow, Scotland, wamekataa kushiriki kwa hoja kuwa ni majeruhi, lakini kukiwa na habari kuwa wamehofia ushindani. 

Baadhi ya wanariadha wa Madola waliokimbia katika mita 10,000, ni Fabiano Nelson ambaye aliweka kambi China, akishika nafasi ya tano kwa muda wa dakika 28:57:96 huku Wilbard Peter aliyeweka kambi Kenya, akishika nafasi ya sita kwa dakika 29:24:30.

Mbio za taifa ni zenye umuhimu mkubwa kwani mbali ya kuibua vipaji vya mchezo huo kila mwaka, pia hutumika kama kipimo cha wanariadha kuelekea  mashindano ya kimataifa kama Madola, Olimpiki na mengineyo.

Licha ya juhudi za mwandishi wa habari hizi kuwapata viongozi wa RT kueleza kisa cha dosari hizo, walionekana kukwepa kwani kila aliyefuatwa alijifanya kuwa na shughuli nyingi uwanjani hapo.

CHANZO Tanzania Daima

Comments

Popular

GIDABUDAY KUHAMASISHA UJENZI WA KIJIJI CHA MICHEZO TANZANIA LENYE JINA YA MWANARIADHA MKONGWE BW.JOHN STEPHEN AKHWARI

Rio Olympics: Brazil win men's volleyball gold, GB's Joyce takes boxing silver – as it happened

Olympics 2016: Usain Bolt completes sprint double, Jade Jones retains taekwondo title

Rio Olympics: Swimmer Lochte apologises for 'robbery' saga