Tunasubiri ‘Matokeo Makubwa Sasa’
Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo bendera yake itapepea
jijini Glasgow, Scotland katika ufunguzi wa Michezo ya Jumuiya ya Madola
itakayofanyika Julai 23 kwenye Uwanja wa Celtic Perth.
Michezo hiyo muhimu hushirikisha nchi wanachama wa
jumuiya hiyo ambazo ziliwahi kuwa koloni la Uingereza na mwaka huu
inatarajiwa kushirikisha mataifa 71 ambayo yatachuana katika michezo 17
tofauti itakayofikia tamati Agosti 3.
Katika michezo hii Tanzania inatarajiwa
kuwakilishwa na wanamasumbwi, wanariadha, kunyanyua vitu vizito, mpira
wa meza, wachezaji judo, waendesha baiskeli na waogeleaji ambao tayari
wameshawasili kwenye kijiji cha michezo nchini Scotland tayari kwa
michezo hiyo. Katika Michezo ya Madola mwaka huu kuna medali 260
zinawaniwa na tunaamini kati ya hizo Tanzania haitaweza kukosa japo moja
kutokana na maandalizi waliyopewa wawakilishi wetu kwenye michezo hiyo.
Watanzania wamechoka kuwa wasindikizaji tena, kama
wa harusi, kwenye mashindano ya kimataifa, hivyo mwaka huu matarajio ya
wanamichezo wetu kufanya vizuri ni makubwa.
Tunafahamu nchi nyingi zinazoshiriki michezo hiyo
zimekuwa na maandalizi kwa wanamichezo wao kwa muda mrefu, lakini hakuna
aliyetukataza na sisi kujiandaa kuzidi wao.
Ni ukweli usiopingika kuwa hakuna nchi inayoshinda
medali kwa miujiza katika michezo hiyo inayoshirikisha mataifa mengi
bali ni maandalizi ambayo tunaamini wanamichezo wetu pia wamefanya vya
kutosha. Hivyo Watanzania wanataka kuona wanamichezo wao wanatwaa
medali, hawataki kubahatisha au wanamichezo wetu kuishia kushiriki na
kurejea kimyakimya.
Msimu huu wa michezo ya 20 ya Jumuiya ya Madola
bila shaka ndiyo msimu wanamichezo watakaopeperusha bendera ya taifa
wakiwa wameandaliwa ipasavyo tofauti na miaka mingine kama ilivyokuwa
2006 na 2010 wakati Michezo ya Madola ilipofanyika Australia na India
ambako wanamichezo wetu hawakupata maandalizi ya kutosha wala kuungwa
mkono ipasavyo na wadau, ikiwa ni pamoja na serikalini.
Safari hii, serikali kwa kutumia uhusiano wake wa
kitamaduni na nchi za China, Uturuki, Ethiopia na New Zealand iliweza
kutuma wanamichezo wake kwenye nchi hizo tofauti kulingana na mazingira
mazuri ya mchezo fulani ili waweze kujiandaa ipasavyo.
Hivyo, tunachokitarajia msimu huu ni medali kwa
wanamichezo wetu 39 waliopo Scotland kwani kwa kufanya hivyo watarejesha
matumaini kwa Watanzania kuendelea kuiunga mkono timu yao inapokwenda
kwenye mashindano makubwa.
Tanzania ina historia na Michezo ya Jumuiya ya
Madola kwa kuwa ndiyo iliyowezesha nchi hii kuvunja medali ya kwanza ya
dunia ya mbio za mita 1,500.
Ni matumaini yetu kuwa wanamichezo wetu watakuwa
na hilo akilini mwao kuwa wanao wajibu wa kuendeleza historia hiyo kwa
kufanya vizuri zaidi na ikiwezekana kuweka rekodi za dunia.
Tunaamini maandalizi waliyoyapata kwenye nchi hizo
yamewaweka vizuri kimchezo na kisaiokolojia na hivyo kilichobakia ni
“Matokeo Makubwa Sasa”.
CHANZO: Mwananchi
CHANZO: Mwananchi
Comments
Post a Comment