Filbert Bayi aishangaa Serikali
Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi
amesema ripoti ya timu za Tanzania zilizoshiriki michezo ya Jumuiya ya
Madola imekwama baada ya Serikali kutaka wanamichezo wote waliokwenda
Scotland kuhusishwa wakati itakapowasilishwa kwao.
Bayi alisema Serikali imetaka wachezaji
walioshiriki kwenye michezo hiyo kuwepo wakati vyama vyao vikiwasilisha
ripoti zao za Madola.
“Ripoti zimechelewa kwa kuwa Serikali imetaka
wanamichezo wote waliokuwa Scotland kuwapo katika kikao cha tathmini,
hiyo ni gharama, hivyo tuko kwenye mchakato wa kutafuta fedha ili
kufanikisha hilo,” alisema.
Alisema gharama za kufanya tathmini hiyo ni Sh 8
milioni, ambazo pia zitatumika kuwagharamia wachezaji wa mikoani
walioshiriki michezo hiyo kuja Dar es Salaam ili kushiriki katika
tathmini hiyo.
“Hii ni mara ya kwanza ripoti ya Madola na
tathmini yake kufanyika kwa kushirikisha wachezaji pia walioshiriki,
inashangaza lakini ndivyo tulivyotakiwa,” alisema Bayi.
Katika michezo hiyo iliyofanyika mwezi uliopita, Tanzania iliwakilishwa na wanamichezo 49, lakini ilirejea mikono mitupu.
SOURCE: Mwananchi
SOURCE: Mwananchi
Comments
Post a Comment