Glasgow: Michezo ya Madola yamalizika
England waongoza, Kenya nao watamba; Mataifa madogo kabisa yaizidi Tanzania |
Michezo ya Jumuiya ya Madola
iliyomalizika jijini Glasgow, Uskochi imemalizika kwa England kuibuka kidedea,
wakizoa jumla ya medali 174, wakifuatiwa an Australia na Canada.
Baada ya siku 11 zilizokutanisha
wanamichezo mbalimbali kwenye michezo tofauti 17, pazia lilishushwa Hampden
Park huku wenyeji wakishika nafasi ya nne, ambayo kwa udogo kijiografia si
haba.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la
Michezo ya Jumuiya ya Madola, Mike Hooper alisema kwamba michezo hii ndiyo
iliyofana zaidi katika miaka 84 ya historia yake. Scotland walipata medali 19
za dhahabu, idadi ambayo hawakupata kutwaa katika mashindano mengine.
Kwa mara ya kwanza katika kipindi
cha miaka 28, England walishika usukani kwa medali 58 za dhahabu, 59 za fedha
na 57 za shaba. Australia walinyakua 49 za dhahabu,
42 za fedha na 46 za shaba huku Canada wakiwa na 32 za dhahabu, 16 za fedha na
34 za shaba.
Nafasi ya tano ilichukuliwa na
India, wakifuatiwa na Newzealand, Afrika Kusini, Nigeria, Kenya na Jamaica
katika nafasi ya 10, wakifunga eneo la kumi bora. Wakati Afrika Kusini, Nigeria na
Kenya wakiitoa kimasomaso Afrika kwa ujumla wake, wapo Watanzania watakaoegemea
kwenye Kenya kufanya vizuri na kuchukulia kwamba ndiyo mafanikio yao.
Hata hivyo, ni vyema ikaeleweka
kwamba katika nchi nyingi zilizofanya vyema, Tanzania ina eneo kubwa na watu
wengi zaidi pamoja na hata vipaji vingi zaidi ya hizo, tatizo ni jinsi ya
kuvikuza tu. Hata nchi ndogo kama visiwa vya Fiji
vinavyokumbwa na misukosuko ya kisiasa imeweza kuwa juu ya Tanzania, pamoja na
Barbados, Samoa, St Lucia isiyosikika kabisa, jirani zetu Zambia, Bahama,
Kiribati ambayo huwezi kuwa hata na wazo ipo wapi kijiografia zote zimetikisa.
Hata Cyprus, Wales, Grenada,
Botswana, Trinidad & Tobago, Ireland Kaskazini, Nauru, Isle of Man
zimefanya kweli, wakati Tanzania haikupata hata medali moja, na kilichoelezwa na
wahusika ni kusubiri ripoti ya wataalamu na kujipanga upya.
SOURCE: Makala ya Israel Saria / Tanzania Sports
Comments
Post a Comment