Ikangaa, Shahanga waishangaa RT
Kanali Mstaafu Juma Ikangaa |
Bingwa wa Afrika wa 1982, Juma Ikangaa na mshindi wa medali
fedha ya Jumuiya ya madola, Gidamis Shahanga wamelishangaa Shirikisho la
Riadha Tanzania (RT) kushindwa kupeleka timu kwenye Mashindano ya
Afrika yanayoendelea nchini Morocco.
Wanariadha hao wakongwe wamesema kuwa, kati ya
vioja vinavyofanywa na RT ni kushindwa kupeleka timu kwenye mashindano
makubwa kama hayo na kusisitiza kuwa kutokwenda kwenye mashindano hayo
kutaiweka Tanzania katika mazingira magumu kwenye Michezo ya Afrika
(All African Games) mwakani.
Gidamis Shahanga |
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti
jana, walisema, Tanzania ilipaswa kutumia mashindano ya Afrika kuwapima
wanariadha wake kwa maandalizi ya Michezo ya Afrika.
“RT imekosea kutopeleka timu Morocco, tunaambiwa
imepeleka wanariadha wawili ambao wamekwenda kuiwakilisha Zanzibar na
si Tanzania bara,” alisema Ikangaa aliyewahi kuwa bingwa wa marathoni
kwenye mashindano hayo ya 1982, nchini Misri.
Wakati Shahanga alisema kuna wanariadha
walioonyesha uwezo mkubwa kwenye mashindano ya taifa, wameshindwa vipi
kuwapeleka kushindana huko? Yale ndiyo mashindano ya kuwajenga
wanariadha kabla hata ya Michezo ya Afrika, Olimpiki, Madola na hata
mashindano ya dunia.
Katibu Mkuu wa RT, Suleiman Nyambui alisema
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imewagharimia wanariadha, Ally Seif na
Mohamed Ibrahim waliopo Marrakech kwenye michuano hiyo ambapo
wanaiwakilisha Tanzania siyo Zanzibar pekee.
“Tanzania bara hatujapeleka mchezaji kutokana na
sababu zisizozulika, hata hivyo waliopo huko wametoka Zanzibar na
wamegharimiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambao wanachuana
kwenye mchezo wa kurusha kisahani, tufe na mkuki.”
CHANZO: Mwananchi
CHANZO: Mwananchi
Comments
Post a Comment