KAULI YA NYAMBUI NI KIPIMO TOSHA CHA UDHAIFU WA UZALENDO WETU
Suleiman Nyambui / Mtanzania asiyejali sheria wala uzalendo |
Kitenge
alikuwa akitaka kujua sababu ya timu ya Tanzania iliyoshiriki michuano ya
Jumuiya ya Madola kurejea nyumbani bila ya hata kipande cha medali.
Nyambui
ambaye katika sauti yake unaweza kubaini mengi, alizungumza mambo ya ajabu
ambayo hauwezi kutarajia kiongozi au mwanamichezo mwenye sifa yake anaweza
kuzungumzia.
Mwanariadha
huyo wa zamani ambaye unaweza kumwita ni kati ya mashujaa waliowahi kuchukua
medali na kuileta nyumbani kupitia michuano ya Olimpiki, alikuwa akizungumza
sawa na mtu aliyekuwa hayuko vizuri, labda kwa uchovu au ni yule asiyejali tu.
Wakati
Kitenge akieleza alitaka kujua kwa nini timu hiyo haikuleta medali, Nyambui
hakufafanua lolote zaidi ya kuhoji vipi Taifa Stars nayo mbona imefungwa na
Msumbiji na kurejea nyumbani mikono mitupu!
Hata aliposisitiziwa
kwamba suala la soka halimhusu na alipaswa kujibu lile linalomhusu, akasema
anashangazwa na watu kuhoji medali wakati hawajui hata muda mzuri waliokimbia
wanariadha waliokwenda Glasgow, Scotland na hicho ndiyo kitu cha kujivunia.
Huyo ni
mwanariadha nyota wa zamani wa nchini, kiongozi wa sasa wa mchezo wa riadha
ambaye anadiriki kuzungumza pumba tena akionyesha hajali na badala ya kufafanua
anachoelezwa, yeye anakwenda kuhoji vipi wengine pia wamefanya vibaya!
Majibu ya
Nyambui yanathibitisha kwamba mafanikio katika mchezo wa riadha sasa ni ndoto,
labda hadi mambo mawili yatokee.
Kwanza
Nyambui aondoke kwenye uongozi wa mchezo huo au soka warudi na kombe nyumbani
baada ya kushinda nje, basi Nyambui ataongeza juhudi kuwajibu.
Anachokisema
anaonyesha hajali kwa kuwa soka hawajashinda, wangeshinda huenda angesikia
wivu. Lakini kwa anachozungumza, inaonyesha wazi kiongozi huyo ni sehemu kubwa
ya tatizo katika mchezo wa riadha.
Sijui
wangapi walimsikiliza Nyambui, lakini kwa waliopata nafasi ya kumsikiliza
‘live’ sijui walitafakari vipi lakini mimi naweka wazi hisia zangu kwamba
ingawa ni mwanariadha wa zamani, anaonyesha kiasi gani asivyo na uchungu na
Tanzania kutofanya vizuri.
Huu ndiyo
wakati mzuri na mwafaka wa wanamichezo au Watanzania kwa jumla kuanza kuhoji na
kuwakemea watu kama akina Nyambui ambao wamejisahau na kugeuza vyama vya riadha
kama mali yao huku wakiamini hakuna mtu anayeweza kuwahoji kutokana na
kinachotokea.
Lazima
tujue kwamba kizuri na kibaya, kinahusisha jina la nchi yetu Tanzania.
Tusiruhusu
watu kama kina Nyambui wakaendelea kuzaliwa wengine ambao watakuwa kila kitu
wanakichukulia kwa urahisi huku wakiona vyama wanavyoviongoza utafikiri ni
mangi anayemiliki duka, hivyo wanaweza kuamua muda wa kufunga na kufungua.
Tunajua
mamilioni ya fedha yamekuwa yakitolewa na mashirikisho ya fedha kwa ajili ya
maandalizi ya michuano mbalimbali ya kimataifa ambayo mwisho wake hatufanyi
vizuri.
Kama hiyo
haitoshi, safari hii serikali kupitia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe, ilitumia fedha za kodi ya Watanzania kwa ajili ya
maandalizi ya timu hiyo ya Jumuiya ya Madola.
Sasa
kuzungumza kama vile unazungumzia familia yako, bila ya kujua Watanzania
wengine wanaumia vipi, si kitu sahihi.
Leo
nakutumia salamu hizi Nyambui lakini nakuasa, kuna haja ya kuonyesha kiasi gani
una uchungu na taifa lako na si kufurahia tu kusafiri na kulala kwenye hoteli
nzuri halafu mnarudi mikono mitupu na maneno mengi ya kujidai yasiyokuwa na
ustaarabu au kuonyesha upevu. Inaonyesha huwa mnajua mtarudi hamna kitu!
CHANZO: Gazeti la Champion
Comments
Post a Comment