Lipumba: Tuwekeze katika michezo
Ni ndoto kwa Tanzania kufanya vizuri kwenye michezo kitaifa na
kimataifa bila kuwekeza kwenye kukuza vipaji vya vijana kama ambavyo
zimefanya nchi nyingine duniani.
Huo ni ushauri wa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi
(CUF), Profesa Ibrahim Lipumba katika mahojiano maalumu na gazeti hili
mwishoni mwa wiki.
Prof Lipumba, ambaye mbali ya kubobea katika
uchumi na siasa, alisema Tanzania haina budi kuwekeza katika michezo
kuanzia elimu ya awali, msingi, sekondari hadi vyuo vikuu ambako vipaji
vipya vitaweza kuibuliwa.
Alisema Tanzania imekuwa ikifanya vibaya kimichezo
kutokana na watoto wake wengi kudumaa kimwili kutokana na lishe duni
kwao na wazazi wao.
“Tunafanya vibaya kimichezo, tunatafuta sababu,
lakini sababu zipo katikati yetu,” alieleza Prof Lipumba na kuongeza
kuwa asilimia 42 ya watoto nchini wamedumaa, jambo ambalo linawaathiri
katika mambo mengi yakiwamo michezo. Msomi huyo ambaye ni shabiki wa klabu ya Simba
alisema uwekezaji ambao umefanywa kwa mfano na klabu ya Azam, ni mfano
mzuri ambao siku za usoni utazaa matunda.
Alishauri Serikali Kuu na hata zile za mitaa
nchini kufikiria namna ya kuyasaidia maeneo yote ambayo yanatoa vipaji
vingi yakiwamo Singida, Arusha na Manyara na kuyasaidia katika kuandaa
wanamichezo bora wa siku za usoni. “Kuna mikoa kama Singida na mingine ni maarufu kwa vipaji katika riadha, tuwekeze pia huko, tuone matokeo yake,” alieleza.
Alishauri klabu mbalimbali za michezo ikiwamo soka
kuangalia mchango wa makocha wazawa ambao wakipewa nafasi wamekuwa
wakifanya vizuri na kuiletea sifa nchi.
CHANZO: Mwananchi
CHANZO: Mwananchi
Comments
Post a Comment