MICHEZO MADOLA: Makocha wajilipua
Makocha wa timu za Tanzania zilizoshiriki na kufanya vibaya
kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola iliyomalizika nchini Scotland
wamefunguka na kueleza masaibu yaliyozisibu timu zao.
Katika kile kinachoonyesha kuwa kimya kingi kina
mshindo, mkuu makocha hao wameeleza mambo mazito ambayo ni vigumu
kuyaamini, lakini ndiyo yaliyozikumba timu za Tanzania. Mojawapo ni jambo ambalo ni hatari kiafya, aibu na
fedheha, likiwamo la mabondia kulazimika kupokezana vikinga ulimi,
hali inayoweza kusababisha maradhi.
Mtaalam mmoja wa michezo, Dk Nassoro Matuzya
alisema jana kuwa kubadilisha vikinga ulimi ni hatari na kiafya
hairuhusiwi, kwani mdomo ni mojawapo ya sehemu zenye bakteria wengi
katika mwili wa binadamu, jambo ambalo ni rahisi kuambukizana magonjwa.
“Wanaofanya hivyo wanapaswa kuwa na wataalam wa
afya ili wawashauri kuhusu madhara yanayoweza kuwapata wanamichezo kwa
kupewa vitu kama hivyo,” alisema na kuongeza kuwa kama kuna timu imewahi
kufanya hivyo, wachezaji wake wapo hatarini kupata magonjwa ya
kuambukiza yakiwamo ya kinywa.
Kwa upande wao, wakizungumza na gazeti hili kwa
nyakati tofauti, kocha wa ngumi, Jonas Mwakipesile na mwenzake wa judo,
Hamis Zaid walidai Serikali haisemi ukweli juu ya ushiriki duni kwenye
michezo hiyo huku mzigo wa lawama baada ya timu kurejea mikono mitupu
wakitupiwa wao.
Makocha hao walisema, Wizara ya Habari, Utamaduni,
Vijana na Michezo imeshindwa kuwaambia ukweli Watanzania kuhusu kile
kilichokuwa kinatendeka kwa timu zao kwenye michezo hiyo iliyomalizika
Agosti 3 nchini Scotland huku lawama zote zikipelekwa kwao (makocha) na
wachezaji.
“Wizara imechangia timu kufanya vibaya, tulifika
Glasgow lakini hadi siku ya ufunguzi wa mashindano, timu hazina vifaa
vya mashindano, wakati tuonaondoka nchini tuliambiwa tutapewa tukifika
huko. “Kilichofanyika tuliletea vikinga ulimi na
protekta chache, tukaambiwa mabondia wapokezane kwani Serikali haina
fedha, hatukuwa na namna zaidi ya kufanya hivyo, kuwaacha vijana
wapokezane vikinga ulimi hivyo, ilikuwa aibu,” alisema Mwakipesile.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa
(BFT), Makore Mashaga kwa upande wake alisema wakati timu inaondoka
ilikuwa chini ya Serikali, hivyo wao hawahusiki na madai kuwa walikuwa
wakipokezana vikinga ulimi. “Sidhani kama Serikali ilishindwa kuwanunulia
vikinga ulimi kwani kimoja kinauzwa Sh10,000 hadi Sh20,000 kutokana na
ubora, protekta moja ni Sh40,000 mpaka Sh50,000 kama walikosa hiyo ni
juu ya Serikali kwani ndiyo tuliikabidhi timu,” alisema.
Naye Hamis Zaid, ambaye aliondoka na timu ya judo
alisema Serikali imechangia wao kufanya vibaya kwani ilishindwa kufanya
majukumu yake kama Serikali kwenye michezo hiyo hali iliyowavunja moyo
wachezaji wake. “Inashangaza, lawama zote tunatupiwa sisi makocha, lakini
Serikali haitaki kusema ukweli nini kilikuwa kinatendeka kule,
tumecheza mashindano kwa kutumia vifaa vya kuazima, siku chache kabla ya
mashindano kwisha ndipo wakatuletea vifaa ili vitusaidie nini,”
alihoji.
Alisema walilazimika kuazima vifaa kwa waandaji
kule Scotland, ambao kiutaratibu kama nchi ikiazima zaidi ya mara mbili
kocha anapewa adhabu ya kugeuka mtazamaji na mchezaji anakwenda ulingoni
peke yake, hivyo dhahama hiyo ilimkumba ambapo mchezaji wake, Amour
Kombo kuingia ulingoni bila sapoti ya kocha. “Mchezaji wangu tegemeo, Ahmed Magogo aliondoshwa
mashindanoni, hakucheza, sababu ni kuchelewa kupima uzito, ukiuliza ni
kwanini aliachwa Tanzania wakati wenzao wanaondoka sababu haijulikani,
hii yote ni ubabaishaji,” alisema.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo kutoka wizara
ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, ambaye pia alikuwa mkuu wa
msafara kwenye michezo hiyo, Leonard Thadeo alipoulizwa jana kuhusu
madai hayo ya makocha alikataa kuzungumzia kilichotokea kwenye michezo
hiyo. “Mimi siwezi kuzungumzia mambo ya Madola, sisi
tuna utararibu wetu, sihitaji kuzungumza chochote kuhusu michezo hiyo
kwenye vyombo vya habari,” alisema Thadeo.
CHANZO: Mwananchi
CHANZO: Mwananchi
Comments
Post a Comment