Viongozi wa michezo nchini ‘janga la Taifa’
Mhe.Dr.Fenella Mukangara / Waziri wa Michezo |
Wakati huo, wanamichezo wa taifa waliaminika kwa
Watanzania kila waliposema wanakwenda kushindana nje ya nchi. Si kama
Tanzania ilishushiwa muujiza bali ilitokana na namna viongozi wa
Serikali na wale wa michezo wa wakati huo walivyotambua wajibu wao. Historia zinaonyesha namna michezo ilivyofanyika
kwa mpangilio kuanzia ngazi za shule, kata, wilaya, mkoa na taifa,
vipaji vilionekana na Taifa likafanya vizuri kimataifa.
Tanzania iling’ara kwenye mashindano ya Olimpiki,
Jumuiya ya Madola na Afrika wakati huo kutokana na namna taifa
lilivyotengeneza timu za ushindani kuanzia ngazi ya wilaya, mikoa na
hata taifa hivyo kuwa na akiba ya vijana wengi wenye vipaji vya michezo. Tofauti na sasa ambapo kadri siku zinavyozidi
kwenda ndivyo jahazi la michezo ya Tanzania linazidi kuzama, hakuna
mchezo wenye afadhali kuanzia kwenye soka, riadha, ngumi, tenisi,
kikapu, netiboli na michezo mingine mingi.
Bila shaka utaungana na mimi na kukubaliana nami
kuwa michezo ya Tanzania sasa iko hoi. Wakati wowote kuanzia sasa
chochote kinaweza kutokea, lakini cha kushangaza hakuna kiongozi hata
mmoja wa michezo anayeonyesha kujali wala kuweweseka na hali hiyo. Kuanzia mamlaka ya juu iliyopewa dhamana ya
kuongoza michezo yaani Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na
kurugenzi zake mpaka wale viongozi wa chini waliopewa dhamana ya
kuongoza michezo, wote wanaonyesha kuridhika na hali iliyopo hivi sasa.
Inashangaza kweli kuona viongozi wa Chama cha
Riadha (RT)wanasimama tena hadharani na kuzungumza kwamba chama hakina
uwezo wa kufanya jambo la maendeleo huku kikidai Serikali kushindwa
kuwasaidia. Pia Wizara inayohusika na michezo inasimama na kusema hakuna
bajeti ya kusaidia michezo kwa kuwa Serikali haina fedha. Hivi kwa
mvutano huu, viongozi hawa walitaka nani aje aionee huruma Tanzania na
kuisaidia ili ifanikiwe katika michezo?, kama viongozi wa michezo hawana
mikakati ya maendeleo wanategemea muujiza gani katika michezo ya
Tanzania?.
Inashangaza Tanzania imebaki kuwa mtazamaji wakati nchi nyingine zikichukua medali kwenye mashindano ya kimataifa. Tumeshuhudia udhaifu wa timu zetu kwenye michezo
ya Jumuiya ya Madola, Olimpiki na hata dunia huku timu yetu ya soka
ikitafuta kwa udi na uvumba nafasi ya kucheza angalau fainali za Mataifa
ya Afrika bila mafanikio.
Tanzania ina wachezaji wengi wenye vipaji na uwezo mkubwa ingawa inaponzwa na mfumo wa uongozi katika sekta ya michezo. Ninapozungumzia mfumo wa uongozi katika sekta hii
namaanisha kuanzia Wizarani, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) hadi
kwenye vyama vya michezo ngazi ya taifa hadi vile vya wilaya.
Wizara kwa nafasi yake inashindwa kutekeleza majukumu yake
katika sekta ya michezo. Inachokifanya ni kuongoza michezo kwa mazoea
kwa viongozi wake kukaa ofisini na kusubiri ripoti.
Vivyo hivyo, BMT inaongoza sekta hiyo kwa mazoea
pia kama vilivyo vyama vya michezo ambavyo viongozi wake wapo ili mradi
wanaitwa viongozi, lakini hawatambui majukumu yao ni yapi katika sekta
hiyo.
Mifumo ya uendeshaji michezo ipo, lakini
haizingatiwi. RT imeshindwa kupeleka wanariadha kwenye mashindano ya
Afrika, tunaona ni kawaida hakuna wa kuhoji. Hali ni kama hiyo BFT.
Kwenye vyama vya mikoa na wilaya pia hakuna
kinachotendeka zaidi ya ubabaishaji. Hali ya viongozi wetu wa michezo
inanipa shaka, Watanzania wamepiga kelele, wameshauri na hata kutoa
madukuduku yao bila mafanikio labda tujaribu njia ya maombi. Lakini ni
vema viongozi wetu wa michezo watangazwe kuwa ni janga kwa viongozi hawa huenda wakabadirika. Maoni 0756 667 666
CHANZO: Mwananchi
CHANZO: Mwananchi
Comments
Post a Comment