Viongozi wa riadha Tanzania wakubali makosa
Tulitegemea Shirikisho la Riadha la Taifa (RT) lingeyatumia mashindano hayo kuanza kutengeneza timu ya ushindani ambayo itashiriki kwenye Michezo ya Afrika mwakani.PICHA|MAKTABA |
Mashindano hayo yalifanyika kwa siku nne, kuanzia
Agosti 10 mpaka 14 huku Afrika Kusini ikiongoza kwa kutwaa medali
nyingi, ikifuatiwa na Nigeria na Kenya.
Katika mashindano hayo, Zanzibar ilipeleka
wanariadha wawili waliochuana katika michezo ya kurusha kisahani, mkuki
na tufe huku Bara ikishindwa kupeleka mkimbiaji hata mmoja. Kitendo cha Bara kushindwa kupeleka wanamichezo
katika mashindano hayo ya riadha ya Afrika kimewanyima fursa wanariadha
kwenda kushindana na kutafuta viwango vitakavyowasaidia kwenye
mashindano mengine ya kimataifa.
Mashindano hiyo ya riadha ni moja ya mashindano
makubwa kwa nchi za Afrika ambayo, ukiondoa Michezo ya Afrika, huenda
ikawa ya pili kwa ukubwa. Michezo hiyo hushirikisha wanariadha wenye
viwango vizuri. Tulitegemea Shirikisho la Riadha la Taifa (RT)
lingeyatumia mashindano hayo kuanza kutengeneza timu ya ushindani ambayo
itashiriki kwenye Michezo ya Afrika mwakani.
Hii ni kwa sababu, kwa kushiriki kwenye mashindano
hayo ya riadha, wanariadha wa Tanzania wangebaini uwezo na viwango vyao
kabla ya Michezo ya Afrika ambayo ni kama Olimpiki ya bara hili
kutokana na ukweli kuwa hushirikisha michezo tofauti.
Tunakumbuka RT iliwaweka kambini wanariadha wengi
kwa ajili ya kujiandaa na Michezo ya Jumuiya ya Madola ya msimu huu na
baadhi yao walishiriki michezo hiyo na wengine waliachwa. Pia kwa kuwa RT ilifanya mashindano ya taifa
katikati ya mwaka huu jijini Dar es Salaam, ingetoa nafasi kwa
wanariadha waliofanya vizuri wangekuw awamekata tiketi ya kushiriki
katika Mashindano ya Riadha ya Afrika.
Tunajua viongozi wa RT wanaweza kujitetea kuwa hao
wanariadha wawili wa Zanzibar waliokwenda Morocco waliiwakilisha
Tanzania kwa ujumla, lakini kwenye mashindano makubwa kama yale taifa
halikustahili kupeleka wanariadha wawili tu kwani Tanzania ina
wanariadha wengi tu.
Sisi tunaamini RT ilitakiwa kupeleka wanariadha
wengi katika mashindano hayo makubwa ya riadha barani Afrika kwa kuwa
yangewasaidia kuwapa mwanga na kuwandaa kwa michezo ijayo. Mara kwa mara tumekuwa tukiwakumbusha viongozi wa
vyama vya michezo nchini kutimiza wajibu wao wa kuendeleza michezo,
lakini katika hali ya kushangaza hilo limekuwa likishindikana.
Viongozi wa RT wameendelea kufanya mambo kwa mazoea na hakuna wa
kuwauliza, tunajidanganya kwamba ipo siku tutafanya vizuri kwenye
mashindano ya kimataifa kwa aina hii ya viongozi wa michezo tulionao.
Sisi tunaamini kuna uzembe mkubwa unafanywa na RT
na hatutakiwi kuufumbia macho kwani tunavyozidi kuchelewa kukemea ndivyo
tunavyozidi kujimaliza katika mchezo wa riadha ambao tulikuwa tukifanya
vizuri miaka ya nyuma.
Kitendo cha RT kushindwa kupeleka wanariadha
katika mashindano hayo ni dalili kwamba tumekubali kuua mchezo wa riadha
nchini, tumekubali kujipoteza kimataifa na tumekubali aibu. Viongozi wa
RT wakubali wamekosea na hivyo kutafuta sababu za kukosea na
kurekebisha.
CHANZO: Mwananchi
CHANZO: Mwananchi
Comments
Post a Comment