Wawakilishi Madola wameifedhehesha nchi
Julai 16, Rais Jakaya Kikwete alimkabidhi Bendera ya Taifa
nahodha wa Tanzania katika Michezo ya Jumuiya ya Madola, Seleman Kidunda
kwa matumani kwamba timu itaipeperusha vyema kwenye michezo hiyo ya 20
iliyofanyika kwenye jiji la Glasgow, Scotland.
Rais alifika Uwanja wa Taifa kwa kazi hiyo, akiwa
na matumaini ya vijana wake kuwa watalinda heshima ya nchi katika
michezo hiyo mikubwa iliyoshirikisha mataifa 71. Kinyume na matarajio hayo, matokeo ndivyo kama
yalivyosikika na kuonekana. Tanzania haikuambulia hata medali moja
katika michezo hiyo ya Madola kama ilivyokuwa kwenye michezo ya 19
iliyofanyika New Delhi, India mwaka 2010.
Katika michezo hii, tunautazama ushiriki wa
Tanzania katika maeneo mawili; maandalizi na ushiriki wa timu zake saba
za riadha, ngumi, kuogelea, mpira wa meza, judo, kunyanyua vitu vizito
na baiskeli.
Katika maandalizi, hakuna ubishi kuwa Tanzania
ilivurunda. Viongozi waliosindikiza timu kwenye michezo ya Madola pamoja
na watu wengine, hawakumwambia Rais Kikwete ukweli wa hali halisi wa
timu zetu.
Wizara ilimpa Rais Kikwete jukumu la kukabidhi
bendera ya Taifa kwa wanamichezo na viongozi waliokwenda kwenye michezo
hiyo, kumbe hakukuwa na ukweli na undani wa uimara wa wanamichezo na
maandalizi yake.
Wanariadha walishindwa kirahisi, mabondia
walipigwa kirahisi na mbaya zaidi kwa mabondia wa Tanzania kusimamiwa na
makocha wa Kenya katika michezo hiyo. Kama kocha aliyemfundisha bondia
hana kiwango, yule anayefundishwa atafaulu? Hivi kweli, kwa staili hii kulikuwa na dalili za
medali? Ilielezwa kuwa makocha wa Tanzania hawakuwa na sifa za
kufundisha mabondia wa michezo hiyo. Kweli hapo tulitegemea medali na
kumpa Rais jukumu la kukabidhi Bendera ya Taifa? Pia tuliambiwa mmoja wa mabondia wetu aliumwa
tumbo na akashindwa kupanda ulingoni na pia ilielezwa kuwa kuna kocha
mmoja alikuwa na kidonda na kushindwa kufanya kazi yake barabara.
Hivi kabla ya timu kuondoka, hayo yote yalikuwa
hayafahamiki? Wakati Rais anakabidhi bendera, wangemwambia tu kuwa
tunakwenda, lakini maandalizi yetu si ya kuleta medali pamoja na kwamba
mmetuweka kambini nje ya nchi miezi miwili, tofauti na sasa wanatoa
visingizio baada ya kurejea.
Ni vyema basi wangemtuma tu mwakilishi wa wizara
kwa ajili ya kukabidhi bendera kuliko kumualika Rais huku wakijua
kulikuwa na kashfa ya uwezo wa ushiriki wa wanamichezo wetu.
Tunaamini kuwa Serikali itataka taarifa ya kina
kuhusu ushiriki wa timu zetu kwenye mashindano hayo, ambayo itaeleza kwa
undani sababu za timu zetu kutofanya vizuri, baadhi ya wanamichezo
kushindwa kutokea jukwaani na masuala mengine yatakayosaidia kusahihisha
pale tulipokosea na kuadhibu pale palipokuwa na uzembe.
CHANZO: Mwananchi
Zaidi ya hayo, tunajua kuwa kuna kashfa hii ya matumizi ya fedha ambayo hadi sasa bado haijatolewa ufafanuzi wa kutosha. Tunaamini katika mashindano kama haya makubwa, timu hupewa malazi kwenye kijiji maalum cha wanamichezo. Hivyo, kiongozi wa msafara hana budi kutoa taarifa
ya nini kililipiwa na Serikali na nini kililipiwa na waandaaji ili
kuondoa hisia za ufisadi katika Dola 93,000 zilizotolewa na kampuni ya
SS Bakhresa kwa wanamichezo.
Tunadhani, ifike hatua viongozi na makocha wawe
wawazi pia vyama viwajibike kwa matokeo mabaya ambayo timu zake zinakuwa
zinapata kwenye mashindano ya kimataifa kama zitashindwa kuandaa timu
mapema. Wachezaji wasishiriki mashindano ya kimataifa ili
mradi bali timu ziwe zimeiva na hata ikitokea tumeshindwa ionekane kweli
tulipambana kuliko ilivyo.Ukweli, viongozi na wasimamizi wa timu za
Tanzania zilizoshiriki Madola wamemfedhehesha Rais. Kwa hayo
yaliyotokea, wanatakiwa wamtake radhi, kiungwana.
CHANZO: Mwananchi
Comments
Post a Comment