Bodi ya ngumi iundwe kunusuru mabondia

Rais wa TPBO Yassin Abdallah 'Ustadhi' akikabidhi vyeti

Mchezo wa ngumi za kulipwa ni miongoni mwa michezo inayoongoza kwa kupendwa hapa nchini, tukiachilia mbali soka ambao unaongoza kupendwa zaidi.

Licha ya mchezo wa ngumi za kulipwa kuwa na nafasi kubwa kwa mashabiki kinachosikitisha ni namna mabondia wa ngumi za kulipwa hapa nchini wanavyotumika kuwaneemesha wengine huku wao wakiambulia fedha ya madafu na wakati mwingine kudhulumiwa kabisa.

Kumekuwa na matukio mengi ya mabondia kudhulumiwa ambayo nikianza kuyaorodhesha huenda ukurasa huu ukajaa na usitoshe, kwani imekuwa ni kawaida viongozi wa ngumi za kulipwa kuwatumia kama

madaraja mabondia. Hiyo yote inachangiwa na mfumo wa uongozi wa ngumi za kulipwa tulionao hapa nchini, japo tunaambiwa ngumi za kulipwa ni biashara, lakini ubabaishaji umekithiri kwa viongozi wake kuendesha mchezo huo wanavyotaka wao.

Huu utaratibu wa ngumi za kulipwa kusimamiwa na kampuni za TPBO Limited chini ya rais wake, Yassin Abdallah ‘Ustadhi’, PST inayoongozwa na Emmanuel Mlundwa sambamba na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC) inayoongozwa na Chaurembo Palasa, ndiyo unaochangia kushusha hadhi ya ngumi za kulipwa hapa nchini.

Wakati TPBC ilipokuwa chini ya utawala wa Onesmo Ngowi, Kamisheni hiyo kidogo ilikuwa inajaribu kufuata kanuni za ngumi za kulipwa kabla ya kupinduliwa na sasa kuongozwa na bondia wa zamani Chaurembo Palasa.

Ubosi wa hawa mabwana watatu kwenye ngumi za kulipwa ndiyo chanzo cha kuvuruga mchezo huo, kwani kila mmoja ana mabavu na anaamua vile anavyojisikia yeye kufanya ilimradi fedha iingie kwenye kampuni yake bila kujali anachokisimamia kina manufaa kwa mchezaji ambaye ni bondia.

Kinachonishangaza ni kwamba waongoza ngumi hawa ambao tulitegemea kuwa mstari wa mbele kuboresha mchezo huo ndiyo wanaoongoza kutengeneza matabaka, migogoro ya wenyewe kwa wenyewe na kudiriki hata kuingia kwenye migogoro na mabondia na mapromota na kusababisha hata kuwastaafisha wengine ngumi bila kupenda.

Hivi karibuni rais wa PST, Emmanuel Mlundwa alisema yeye ndiye aliyemuweka Palasa TPBC na uwezo wa kumng’oa pia anao endapo akitaka huku akiungwa mkono na mwenzake wa TPBO ambao walikuwa mstari wa mbele kuhakikisha Ngowi anaondoka kuongoza TPBC ili Palasa aingie.

Kauli hiyo ilinipa wasiwasi, hivi viongozi wachache wanakuwa na kiburi kiasi hiki kwenye ngumi za kulipwa, haki ya bondia itakuwa wapi? Kumekuwa na ubabaishaji uliokithiri kwenye ngumi za kulipwa na hiyo yote inatendeka kwa kuwa tu PST, TPBO na TPBC zinaongoza ngumi kwa jeuri, kiburi na kufanya zinavyojisikia kwa kuwa tu hakuna mahali zinapowajibika.

Tena kwa jeuri waliyokuwa nayo wanadiriki hata kutoa majibu yasiyofaa hata pale wanapoulizwa juu ya madudu wanayofanya kwenye ngumi za kulipwa. Sasa kinachonipa maswali hivi vyama vinasimamia nini? je, vina msaada gani kwa mabondia wanaosababisha wao wawe kazini?.

Kwa mtindo huu unaotumiwa na viongozi hawa wa ngumi za kulipwa, mchezo huo hauna muda mrefu hapa nchi utapoteza sifa na hadhi yake kama hatua za makusudi hazitachukuliwa mapema. Ndiyo maana naona kuna haja sasa ya kuundwa bodi ya kusimamia ngumi za kulipwa ili kuunusuru mchezo huu tofauti na sasa kiongozi mmoja anafanya anavyojisikia.

Kama itaundwa bodi ya kusimamia ngumi za kulipwa, kazi yake itakuwa ni kuvisimamia vyama hivi vya ngumi za kulipwa nchini ambavyo ni PST, TPBO na TPBC.

CHANZO: Mwananchi

Comments

Popular

GIDABUDAY KUHAMASISHA UJENZI WA KIJIJI CHA MICHEZO TANZANIA LENYE JINA YA MWANARIADHA MKONGWE BW.JOHN STEPHEN AKHWARI

Rio Olympics: Brazil win men's volleyball gold, GB's Joyce takes boxing silver – as it happened

Olympics 2016: Usain Bolt completes sprint double, Jade Jones retains taekwondo title

Rio Olympics: Swimmer Lochte apologises for 'robbery' saga