Sugu atikisa Uwanja wa Sokoine
Sugu sugu sugu… hivyo ndiyo mashabiki wa Mbeya City walivyoimba
kwa muda mrefu baada ya mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi
‘Sugu’ kuingia uwanjani juzi kushuhudia mechi ya Ligi Kuu kati ya Mbeya
City na Coastal Union.
Ilikuwa katika dakika ya 38 ya mchezo huo, wakati
Sugu alipoingia uwanjani na baada ya kushuka tu kwenye gari lake, uwanja
mzima ulizizima kwa kelele za mashabiki kumshangilia kwa nguvu zote
wakisema “Sugu sugu sugu”, huku wakimtaka aende kukaa kwenye eneo
walilokuwapo. Sugu alilikubali wito huo na kwenda kukaa eneo la
mashabiki hao.
Mmoja wa viongozi waliokuwa kwenye jukwaa kuu
alishuka ghafla kwa lengo la kumkaribisha Sugu meza kuu, lakini Sugu
hakwenda na badala yae alinyosha njia kwenda kukaa kwa mashabiki huku
akishangiliwa kwa nguvu.
Akizungumza na gazeti hili, baada ya kumalizika
kwa mechi hiyo, Sugu alisema hakuwa na sababu yoyote ya kukaa jukwaa kuu
kwani uhondo wa mchezo ni pale unapokuwa na vijana aliowaita wenye
‘mizuka’.
“Utaendaje kukaa jukwaa kuu wakati masela wenye
mizuka wapo na raha. Michezo ni mizuka ya mashabiki hivyo ni lazima
nikajumuike nao kuishangilia timu yetu,” alisema Sugu.
Kabla ya mechi hiyo kuanza, mamia ya mashabiki wa
Mbeya City walifanya maandamano yasiyokuwa rasmi na kufunga barabara kuu
ya Dar es Salaam - Zambia wakati wakielekea kushuhudia mechi hiyo
kwenye Uwanja wa Sokoine.
Mashabiki hao walikusanyika kwenye kituo cha
daladala cha Kabwe kuanzia saa 7:00 mchana, walianza msafara saa 9:05
alasiri wakiwa kwenye mabasi matano wengine wakitembea wa miguu.
Walitumia takribani saa moja kufika uwanjani.
CHANZO: Mwananchi
CHANZO: Mwananchi
Comments
Post a Comment