Sumaye: Tulikosea kufuta michezo shuleni

Frederick Tluway Sumaye/Waziri Mkuu Mstaafu
Waziri Mkuu Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye amesema uongozi wao ulikosea kimsingi kufuta michezo shuleni. Mwishoni mwa 1996, Serikali kupitia aliyekuwa waziri mwenye dhamana ya michezo, Joseph Mungai ilipiga marufuku michezo yote kwenye shule za umma.

Katika tangazo lake, Mungai ambaye alikuwa Mbunge wa Mufindi Kaskazini (CCM), alisema uamuzi huo ulichukuliwa ili kuepusha muda mwingi wa masomo uliokuwa ukipotea kwa wanafunzi kushiriki michezo.
Mungai alieleza wakati ule kuwa wanafunzi nchini walihitaji muda wa saa 198 kwa ajili ya masomo kwa mwaka, lakini nyingi kati ya hizo zilipotea bure kwenye shughuli nyingine, zikiwamo michezo.

Lakini, akizungumza na gazeti hili kwenye mahojiano maalumu nyumbani kwake, Kiluvya, wilayani Kisarawe, mkoani Pwani, Sumaye aliukosoa uamuzi huo. “Lazima nikiri kuwa ‘tuli-overreact’ (tulitoa uamuzi mkubwa mno) kufuta michezo katika shule zetu,” alisema Sumaye, ambaye anajianisha mwenyewe kuwa mwanamichezo.

Alisema yeye ni mpenzi wa timu yoyote inayofanya vyema katika michezo, ingawa binafsi amekuwa akifahamika kuwa shabiki wa Simba. Aliongeza kuwa ingefaa michezo iendelee katika shule zote, ila kwa kuzingatia uwiano wa muda ambao unatumika katika kutoa taaluma na kucheza na kuongeza kuwa michezo inaweza kuisaidia Tanzania kujitangaza.

“Kimsingi, tulitakiwa tufahamu kuwa michezo pia ina umuhimu wake kwa ustawi na maendeleo ya nchi yetu, wala si kuiondoa kijumla,” alisema. Aliongeza: “Tungeangalia aina ya michezo kwani inao umuhimu kwa maendeleo ya nchi, hata kujenga afya, miili na akili za vijana wetu.”

Alisema walisikia malalamiko ya baadhi ya wazazi, walezi kwamba vijana wao walikuwa wakipoteza muda kushiriki michezo tangu ngazi ya elimu ya msingi, sekondari hadi vyuo, jambo ambalo lilisababisha michezo yote kufutwa katika mtalaa wa masomo.

Alisema makosa hayo bado yanamsumbua hadi leo, ingawa anajivunia ujenzi wa Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 60,000. “Ninakumbuka Mzee Mkapa (Benjamin) aliwaahidi wanamichezo kuwajengea uwanja wa kisasa wa michezo na uamuzi wake akautimiza.

“Katika hili la uwanja, Mzee Mkapa aliahidi, sisi tulikuwa watekelezaji wake,” alisema na kuongeza kuwa alikwenda China kwa mazungumzo na serikali ambayo ilikubali kuipa mkopo Tanzania kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huo.
Kuhusu michezo kwenye serikali za mitaa, idara ambayo inasimamiwa na ofisi ya Waziri Mkuu, Sumaye alisema wakati wao walihakikisha fedha zao zinatengwa kwa ajili ya maendeleo ya michezo kwenye ngazi hizo za utawala wanchi.

Hata hivyo, katika siku za karibuni kumekuwa na madai kwamba halmashauri nyingi hazipewi tena fungu la fedha kwa ajili ya michezo, jambo ambalo hata hivyo, Sumaye anaeleza kuwa linaweza kutokea kutokana na ukosefu wa fedha.

Zilivyo sekta nyingine, sekta ya michezo ni chanzo kikubwa cha mapato, lakini nchini mwetu inaonekana michezo siyo chanzo cha mapato na hata wanamichezo hawana thamani ile wanayostahili. Mbali ya shughuli za uongozi, Sumaye anaeleza kuwa alishiriki kila siku kufanya mazoezi ya viungo pamoja na timu mbalimbali za michezo wakati wote wa vikao vya bunge mjini Dodoma.

Alisema ofisi yake na ile ya bunge kwa nyakati tofauti walizialika kwa nia ya kuzipongeza timu zote za michezo mbalimbali zilizofanyika vyema kwenye michezo kitaifa na kimataifa.

CHANZO: Mwananchi

Comments

Popular

GIDABUDAY KUHAMASISHA UJENZI WA KIJIJI CHA MICHEZO TANZANIA LENYE JINA YA MWANARIADHA MKONGWE BW.JOHN STEPHEN AKHWARI

Rio Olympics: Brazil win men's volleyball gold, GB's Joyce takes boxing silver – as it happened

Olympics 2016: Usain Bolt completes sprint double, Jade Jones retains taekwondo title

Rio Olympics: Swimmer Lochte apologises for 'robbery' saga