Tufanye sensa ya vyama vya michezo nchini
Dioniz Malinzi / Bosi wa Baraza la Michezo Tanzania |
Kimsingi, Tanzania imeharibu na kutia aibu kuanzia soka, ambayo ndiyo mchezo maarufu, hadi michezo mingine.
Viongozi wenye dhamana katika michezo na wao
wanaingiza siasa badala ya kuangalia nini wajibu wao na kwa chama na
manufaa ya taifa. Tumewahi kupiga kelele sana katika eneo la michezo
kuwa udhaifu wa uongozi na hasa kwa kutokuwa na dhamira na dira ya
maendeleo, ndiyo kunachangia kutopiga hatua.
Kuvurunda kwa wanamichezo wa Tanzania katika
mashindano mbalimbali, kutokana na kukosa umakini na zaidi ni udhaifu wa
uongozi katika vyama na klabu. Kwa jinsi hiyo, itachukua muda mrefu Tanzania kupiga hatua katika michezo kama mfumo wa utendaji ndani ya vyama hautabadilika.
Kutokana na msingi huo, kuna haja kwa mamlaka
inayohusika na michezo yote kufanya sensa ya vyama vya michezo ili kujua
hadi sasa kuna vyama vingapi vilivyo hai na vina mahitaji gani. Mamlaka hizo ni Msajili wa Vyama vya Michezo,
Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kurugenzi ya Michezo na juu zaidi ni
wizara yenye dhamana na michezo.
Katika kufanikisha hili, iangaliwe, riadha
wanafanya nini, nini programu yao ya mwaka? Je inatekelezwa? Nini
matatizo na mafanikio, hivyo hivyo katika soka, netiboli, mpira wa
mikono, wavu, ngumi, baiskeli, kikapu, kuogelea, skwashi na michezo
mingine mingi. Kila mara tunasikia kuna uchaguzi katika vyama vya
michezo, wanachagua viongozi, lakini je, ni kweli wanaoingia madarakani
wana dhamira ya kweli ya kuendeleza mchezo husika?
Vyama hivi vyote ni vya kufanyia sensa ili kujua
kama viko hai, vinaendeshwa kwa kufuata katiba, vyanzo vyao vya mapato
ni nini, na vinahitaji msaada gani, na zaidi ya yote Serikali inawezaje
kuvisaidia. Tuliona jinsi Serikali ilivyoshikia bango suala la
mabadiliko ya katiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), na kudiriki
hata kutaka kuvunja uongozi. Serikali inafanya nini kwa vyama vingine
ambavyo havina hata katiba? havifanyi uchaguzi na wala havina hata
utunzaji mzuri wa mapato yake?
Tunapata wasiwasi kwamba Serikali huingilia pale tu viongozi
wake wanapokuwa na maslahi yao, na si kwa lengo la kuhakikisha vyama
vinaendeshwa kidemokrasia.
Hivi sasa kuna chama kama Chama cha Wavu Tanzania,
au mpira wa mikono, lakini havina mashindano kwa mwaka mzima. Havina
hata ligi. Serikali haioni hilo?
Leo tuna wanamichezo wa kuogelea walioenda
Scotland kwenye Michezo ya Madola. Hawa walipatikana vipi wakati hakuna
mashindano ya kuogelea nchini? Serikali haina budi kuibuka na ikiwezekana
kuangalia upya majukumu yake katika usimamizi wa vyama vya michezo na
michezo kwa ujumla. Kama majukumu hayo yamepitwa na wakati, basi haina
budi kujiangalia upya na kuyarekebisha ili yaende na wakati.
Mfumo wa siasa umebadilika sana tangu sheria
iliyounda Baraza la Michezo ilipopitishwa na hivyo, lazima imepitwa na
wakati sana. Kwa hiyo, kama Serikali itafanya sensa hiyo ya vyama, pia
itathmini majukumu yake katika usimamizi wa michezo. Kauli hiyo ya maandalizi imekuwa ikitolewa kila
mwaka, lakini hakuna jipya linalofanyika. Mambo ni yaleyale, viongozi
wanashtuka dakika za mwisho kuandaa timu bila kujali ukubwa na umuhimu
wa mashindano.
Maandalizi yanafanywa tu kama kielelezo kwamba
yalikuwapo kabla ya timu au washiriki kwenda kushindana kushindana
kimataifa, lakini siyo kwa lengo la kuhakikisha tunafanya vizuri. Ndiyo maana tunaona sensa itasaidia kujua vyama
mfu na hai. Watanzania wanatamani kuona wanamichezo wake wanafika mbali
katika kila hatua za mafanikio, lakini hawa walio na dhamana hawataki.
Wakati Michael Yombayomba alipotwaa medali ya
Madola mwaka 1998 katika ngumi, alilakiwa kwa shangwe na nderemo za
kutosha, ni kwamba Watanzania wanapenda mafanikio, Watanzania wana hamu
ya mafanikio, lakini hawa waliopewa dhamana ni tatizo. Kimsingi, tunaona kuna haja ya kufanya sensa ya
vyama vya michezo hai, viongozi ‘hai’, Katiba hai ili walau kuanza
kufufua michezo Tanzania.
CHANZO: Mwananchi
CHANZO: Mwananchi
Comments
Post a Comment